
Al Duhail anayochezea Olunga yaaibishwa Klabu Bingwa Asia 7-0
Na GEOFFREY ANENE
MIAMBA wa Qatar Al Duhail wameaibishwa 7-0 kwenye Klabu Bingwa Asia mikononi mwa mabingwa watetezi Al Hilal katika nusu-fainali ugani Al Thumama, Jumapili.
Al Duhail ya kocha Hernan Crespo iliyoingia mechi hiyo na rekodi duni dhidi ya klabu hiyo kutoka Saudi Arabia ya ushindi mmoja, sare tatu na vichapo viwili, ilionekana kuzidiwa maarifa kutoka dakika ya kwanza.
Klabu hiyo almaarufu Purple Knights ilijipata chini mabao mawili ndani ya dakika 10 za kwanza baada ya mshambulizi wa zamani wa Watford na Manchester United Odion Ighalo kutetemesha nyavu dakika ya pili na 10.
Mambo yaliharibika pale Moussa Marega aliongeza bao la tatu dakika ya 13. Shuti kali kutoka kwa mvamizi matata wa Kenya, Michael Olunga ilipanguliwa na kipa Abdullah Al Muiauof sekunde chache baadaye.
Al Hilal iliendelea kuhangaisha Al Duhail kwa kutumia kasi ya kutisha na haikuwachukua muda kuongeza bao la nne kupitia kwa Marega dakika ya 26 baada ya kupokea mpira kutoka kwa kipa wake.
Almayuof kisha alipangua kombora jingine kutoka kwa Olunga dakika ya 33 kabla ya Al Duhail kuponea tundu la sindano kuongezwa bao baada ya shuti la Salem Al Dawsari kupoteza nafasi ya wazi alipobaki pekee yake na kipa Salah Zakaria.
Marega kisha alisuka pasi kwa kutumia kisigino chake iliyokamilishwa na Al Dawsari.
Mshambulizi huyo wa Mali aliyewahi kuchezea Porto alinyimwa bao la tatu baada ya kupatikana ameotea dakika ya 40.
Mshambulizi wa Nigeria Ighalo alipata goli lake la tatu katika kipindi cha pili baada ya kuadhibu Al Duhail kwa pasi mbovu.
Ighalo alihitimisha dakika ya 61 kabla ya Olunga kupumzishwa dakika ya 67.
Kocha wa Al Duhail, Hernan Crespo alikuwa amebashiri kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu sana kwa vijana wake. Kabla ya kichapo cha Jumapili, Al Duhail ilikuwa imepokea kipigo kikubwa cha 5-0 dhidi ya Al Ain kutoka Milki za Kiarabu katika mechi ya makundi mwaka 2014.
Source link