
Aliyeua mpenzi kwa shoka asema alikerwa kwa kuitwa ‘mfupi’
TITUS OMINDE Na ANNEBEL OBALA
MSHUKIWA wa mauaji wa mwanafanzi wa Chuo Kikuu cha Moi Ivy Wangeci, 22, miaka mitatu iliyopita, Ijumaa alikiri kuwa alimkata kwa shoka baada ya kusalitiwa kimapenzi.
Naftali Kinuthia alieleza Mahakama Kuu ya Eldoret kuwa alikasirishwa na usaliti huo akidai kuwa Bi Wangeci, ambaye alikuwa akisomea kozi ya matibabu, alikuwa na mpenzi mwengine.
Siku ya tukio, Kinuthia alieleza korti kuwa alizidiwa na wivu kumwona mpenzi wake akimkumbatia mwanaume kwa furaha mbele yake.
Mbele ya Jaji Stephen Githinji, wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, alisema alishindwa kuvumilia usaliti huo ndiposa akamkata mpenziwe kwa shoka.
“Singeweza kuvumilia ndipo nikapandwa na hasira na kumkata kwa shoka. Sikujijua wakati huo,” akasema Kinuthia.
Ingawa hivyo, alisema pia hasira yake ilikuwa juu kwa sababu alikuwa ametumia pesa nyingi wakati wa uhusiano wao na Bi Wangeci ila marehemu hakumwambia kuwa ana mpenzi wa pembeni.
Alisikitikia mauti ya mwenzake na kusema kuwa tofauti hizi zingesuluhishwa kwa njia nyingine ambayo haingeishia kifo.
Naftali akifunguka na kusema kuwa shoka ambalo alitumia kumuua marehemu lilikuwa ya kujilinda wala hakulenga kulitumia kwa mauaji. Hata hivyo, alisisitiza kuwa alijaribu juu chini kuhakikisha kuwa uhusiano wao unarejea kuwa dhabiti licha ya kwamba marehemu naye aliendelea kumtelekeza.
Aidha alimpa marehemu Sh7,000 kutumia wakati wa sherehe ya kuzaliwa kwake kati ya bajeti ya Sh14,000 ambazo alikuwa akitaka. Akimjibu wakili wa upande wa mashtaka Jackson Ndegwa, Naftali alisikitika kuwa hakuwa na lengo la kumuua Bi Wangeci licha ya kumwonyesha dharau na kumwambia hamtaki tena kimapenzi.
“Niliendelea kumtumia pesa licha ya uhusiano wetu kuendelea kuwa na doa na hata akanizuia kumfikia kwa simu. Nilikuwa na nia ya kuhakikisha kuwa mapenzi yetu yananawiri wala sikuwa na nia ya kumuua,” akaeleza mahakama.
Hata hivyo, Naftali alishangaza mahakama baada ya kudai aliwataka wazazi wa Bi Wangeci wamrejeshe pesa zake ambazo zilikuwa zaidi ya Sh100,000 alizotumia kwa mwana wao.
Licha ya kwamba alichangia sherehe hiyo, ilisikitisha kuwa hakualikwa na siku ya tukio alikuwa amesafiri kuanza kufanikisha sherehe yenyewe.
Kitumbua kiliingia mchanga baada ya Naftali kuelezwa na Bi Wangeci kuwa alikuwa mfupi na hakuwa akimpenda.
Wawili hao walianza uhusiano wao wa kimapenzi katika shuke ya msingi ya Thika Mjini na wakaendelea hadi shule ya upili ambapo Bi Ivy alikuwa shule ya wasichana ya Alliance huku Kinuthia akiwa Nyandarua Excessive.
Kusikilizwa kwa kesi hiyo kukiendelea, Naftali amekuwa akizuiliwa katika gereza la Eldoret baada ya kukanusha kuwa alimuua Bi Wangeci miaka mitatu iliyopita.
Source link