
Benki kuchunguzwa kwa kufyonza akaunti za wateja
NA MARY WANGARI
SERIKALI huenda ikaanzisha uchunguzi dhidi ya benki mbalimbali nchini kuhusiana na madai ya uporaji wa pesa kwenye akaunti za wateja kufuatia pendekezo lililowasilishwa na Bunge la Seneti.
Seneti imeagiza Kamati ya Fedha na Bajeti, “kuchunguza madai ya utowaji pesa kinyume na sheria kutoka kwenye akaunti zinazomilikiwa na wateja katika benki mbalimbali nchini.”
Pendekezo hili limejiri wakati ambapo Kenya imegubikwa na malalamishi mengi kutoka kwa wateja wa benki baada ya pesa kutoweka kwenye akaunti zao huku baadhi wakiachwa maskini hohehahe.
Akiwasilisha rasmi pendekezo hilo mnamo Jumatano, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti, Tabitha Mutinda, alirejelea malalamishi kadhaa ya wateja kuhusiana na benki mbalimbali nchini.
“Ninasimama kuambatana na Kanuni za Seneti Kifungu 53(1), kuitisha taarifa kutoka kwa Kamati ya Fedha na Bajeti kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyohusu akaunti mbalimbali za wateja katika benki za Kenya,” alisema Mbunge huyo Maalum.
“Tunataka kuangazia masuala haya kwa kina na kuelewa matatizo yalianzia wapi ili tuweze kupata suluhisho la kudumu na la muda mfupi kuhusu matatizo haya. Inasikitisha kwa kweli.”
Benki ya Fairness imemulikwa zaidi kwenye mchakato huo huku ikiandamwa na malalamishi mengi kutoka kwa wateja katika matawi yake mbalimbali nchini na hata katika mataifa jirani.
Seneta huyo alirejelea kisa ambapo akaunti ya Benki ya Fairness, Tawi la Gikomba inayomilikiwa na mteja kwa jina Marion Nyambura Karanja, inasemekana kufagiliwa kiasi cha zaidi ya Sh700,000.
Katika kisa kingine vilevile, pesa za uzeeni za Bw Matthew Mathia zilizotolewa kwenye akaunti yake ya Benki ya Fairness, Tawi la Limuru, zilitumika kulipia mkopo uliokuwa umechukuliwa kinyume na sheria kupitia akaunti.
“Eleza hatua zilizochukuliwa na Benki ya Fairness kuhusu kuwafidia wateja wake, hususan visa vya Marion Nyambura Karanja ambaye akaunti yake ya Tawi la Gikomba ilifagiliwa zaidi ya Sh 700,000, Matthew Mathia ambaye pesa zake za uzeeni zilitumika kulipia mkopo uliochukuliwa kinyume na sheria kupitia akaunti yake katika Tawi la Limuru na visa vingine vingi sawa na hivyo katika matawib ya benki hiyo nchini Uganda,” ilisema taarifa.
Seneti imeagiza wakurugenzi wa benki mbalimbali zilizohusishwa na visa hivyo, Mkuu wa CBK na Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu katika Taasisi za Benki kufafanua mikakati iliyowekwa kukomesha visa kama hivyo vya wizi na kuondoa shaka kuhusu mifumo ya ulinzi kwenye benki.
“Orodhesha hatua, iwapo kuna yoyote, iliyochukuliwa na benki ambapo madai kama hayo yamewahi kutajwa hapo mbeleni, ili kuhakikisha kuwa wateja ambao huenda walipoteza fedha zao kupitia visa kama hivyo vya uhalifu, wamefidiwa,” alisema.
Source link