
Bunge hatarini kuwa mateka wa serikali
NA BENSON MATHEKA
BUNGE liko katika hatari ya kupoteza uhuru wake na kugeuka mateka wa serikali, huku Rais William Ruto akifanya kila juhudi kulidhibiti alitumie kutekeleza ajenda zake.
Ili kuafikia hayo, Rais Ruto amechukua hatua za kupunguza nguvu za upinzani kwa kuvutia wabunge wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, na wale huru upande wake na kuhakikisha wandani wake wanasimamia kamati muhimu.
Ni Rais Ruto aliyechagua viongozi wa kamati bungeni katika mikutano aliyofanya na wabunge na maseneta wa Kenya Kwanza kabla ya Bunge la 13 kuanza vikao vyake.
Kiongozi wa nchi amekuwa akisisitiza kuwa, yuko tayari kushirikiana na viongozi waliochaguliwa bila kujali mirengo ya kisiasa.
Tayari, wabunge wapatao 30 wa chama cha Jubilee ambacho ni mojawapo ya vyama tanzu vya Azimio, wametangaza kuwa watashirikiana na Rais Ruto na kuunga sera za serikali Bungeni.
Rais Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua, pia wamekutana na baadhi ya wabunge wa chama cha ODM katika juhudi za kuwataka kuunga ajenda za serikali katika Bunge.
Iwapo wabunge hao wa Jubilee na ODM na wale huru wataungana na Kenya Kwanza, wanaounga serikali watakuwa 231 wakiwa wnaapungua wawili kuweza kutimu 233, idadi inayohitajika kupitisha maamuzi muhimu, ikiwemo kubadilisha katiba.
Katika hatua inayoonyesha Bunge limepoteza uhuru wake, mnamo Desemba 9 2022, Rais Ruto aliandikia Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi, akipendekeza mabadiliko katika Katiba ambayo yatahitaji awe na idadi kubwa ya wabunge kupitishwa.
Wadadisi wa siasa wanasema hii ndiyo sababu ambayo imefanya kiongozi wa nchi kuhakikisha ana idadi kubwa ya wabunge wanaounga ajenda zake.
Rais Ruto hakuficha nia yake alipokutana na wabunge wa Jubilee katika Ikulu ya Nairobi mwezi jana akisema anawachukulia kama wanachama wa mrengo wake.
“Mumefanya maamuzi sahihi kwa kuwa Kenya ni nchi ya demokrasia, sasa nyinyi ni wanachama wetu na kuendelea mbele tutawachukulia kuwa wanachama wetu, nitawategemea katika kushinikiza ajenda za serikali katika Bunge la Taifa na Seneti,” Dkt Ruto alisema.
Wadadisi wanasema baada ya kuhakikisha maspika wa mabunge yote mawili walikuwa washirika wake, alichobakisha kudhibiti Bunge ni idadi kubwa ya wabunge na maseneta ambayo ameonekana kutimiza kwa kuwinda wale wa upinzani na kufifisha nguvu zake.
Wandani wa Rais Ruto pia wanaongoza kamati zenye ushawishi katika Bunge huku maspika wakionekana kutokuwa na uhuru wa kufanya maamuzi ya wazi ikiwemo kukubali mabadiliko ya uongozi wa wachache.
Mnamo Februari 14, Bunge la Taifa lilikataa kubadilisha wanachama wa Kamati ya Shughuli za Bunge, uamuzi ambao ulifanya Kenya Kwanza kuwa na idadi kubwa ya wanachama wa kamati hiyo muhimu.
Hii inamaanisha kuwa, wanachama wa Jubilee katika kamati hiyo waliopaswa kuwa upande wa Azimio wataendelea kuhudumu wakiwakilisha maslahi ya Kenya Kwanza.
Mwezi jana, Naibu Spika wa Seneti alichelea kuidhinisha mageuzi ya uongozi wa wachache baada ya kiongozi wa Azimio Raila Odinga kubandua maseneta waliokutana na Rais Ruto.
“Ninaamini kuwa Rais wa Kenya William Ruto anataka mfumo wa serikali wa Bunge,” asema Seneta wa Narok Ledama Ole Kina, akirejelea juhudi za Kenya Kwanza za kuwinda wabunge wa upinzani.
Source link