
Cleophas Malala ateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa UDA
NA MARY WANGARI
ALIYEKUWA Seneta wa Kaunti ya Kakamega, Cleophas Malala, sasa ndiye Katibu Mkuu mpya wa chama tawala cha Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA).
Bw Malala amechukua usukani kutoka kwa Mbunge Maalum Veronica Maina katika uongozi wa UDA, baada ya kutema Amani Nationwide Congress (ANC) cha Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, na kujiunga na kambi ya Rais Ruto.
“Nimepokea uteuzi huu kama Katibu Mkuu wa pili wa chama tawala. Namshukuru Mola na kiongozi wa chama chetu kwa fursa hii,” alisema Bw Malala.
Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa Jumatatu kwenye chama tawala, Gavana wa Embu Cecily Mbarire vilevile aliteuliwa kama mwenyekiti wa UDA, huku akichukua nafasi ya Bw Johnson Muthama.
Bw Muthama alijiuzulu ili kutilia maanani uteuzi wake kama mtumishi wa umma.
Aidha, aliyekuwa seneta wa Mombasa, Hassan Omar aliteuliwa kama Naibu Mwenyekiti wa UDA huku akimrithi Bw Kipruto Kirwa.
Bw Japheth Nyakundi alichukua usukani kutoka kwa Bw Omingo Magara kufuatia uteuzi wake kama Mweka hazina mpya.
Bw Vincent Munyaka atahudumu kwa muda kama katibu wa maandalizi kabla ya chaguzi.
Source link