Friday, March 3, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsDeni la maziwa ya Sh71m latia kaunti ya Mombasa mashakani – Taifa...

Deni la maziwa ya Sh71m latia kaunti ya Mombasa mashakani – Taifa Leo

Deni la maziwa ya Sh71m latia kaunti ya Mombasa mashakani

Deni la maziwa ya Sh71m latia kaunti ya Mombasa mashakani

NA PHILIP MUYANGA

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa, imeshtakiwa kwa madai ya kutolipa Sh71.3 milioni kwa muungano wa vyama vya ushirika uliosambaza maziwa shuleni kaunti hiyo.

Meru Central Dairy Cooperative Union Ltd, ambayo ilikuwa imeshinda zabuni ya kusambaza maziwa kwa shule za kaunti hiyo kuanzia Machi 2019 wakati wa utawala wa aliyekuwa gavana Hassan Joho, inatafuta agizo la kulazimisha serikali ya kaunti hiyo kulipa pesa hizo pamoja na riba.

Katika ombi lake katika Mahakama Kuu mjini Mombasa, muungano huo unasema wafugaji kadhaa sasa wamesusia kuuzia muungano huo maziwa kwa sababu ya deni hilo na hivyo basi kukwamisha shughuli zake.

Muungano huo unasema, ili kuendelea na shughuli zake licha ya serikali ya kaunti kutolipa pesa za shule tangu 2019, ilibidi kupata ufadhili kutoka kwa taasisi za kibiashara na wakopeshaji wengine ambao sasa wanatishia kuuza mali zao ili kujilipa madeni yao.

“Iwapo watatimiza vitisho vyao, muungano unaweza kuwa kwa hatari ya kufilisika,” unahoji muungano huo.

Hata hivyo, kupitia kwa wakili Murtaza Tajbhai, serikali ya kaunti ilitaja ombi la muungano huo kuwa lisilo na msingi, la kipuuzi na kupoteza muda wa mahakama na kutaka litupiliwe mbali.

Bw Tajbhai pia anahoji katika mawasilisho yake kwamba hitaji la malipo halikuwasilishwa kwa afisa mhasibu wa kaunti.

“Hakuna ushahidi uliotolewa na mlalamishi kwamba aliwahi kudai malipo ya kiasi hicho,” inahoji serikali ya kaunti.

Kulingana na serikali ya kaunti, waziri wa fedha katika kaunti ndiye hutoa maamuzi ya fedha lakini muungano haujamtaja kama mshtakiwa katika malalamishi mahakamani.

Muungano huo umelalamika kuwa, pesa hizo bado hazijalipwa hata baada ya kutambuliwa na serikali ya kaunti kupitia hati ya kukiri deni.

“Mahakama ilitoa amri na ilitolewa kwa washtakiwa ambao wamepuuza maagizo ya korti waziwazi, walishindwa kutii na kukataa kulipa deni ipasavyo kwa mlalamishi,” mawasilisho mahakamani yanasema.

Muungano huo pia umelalamika kuwa zaidi ya wafugaji 30,000 wako hatarini kupigwa mnada kwa sababu ya deni hilo.

Pia unahoji kuwa serikali ya kaunti ina uwezo wa kulipa deni lakini imechagua kujificha nyuma ya vijisababu kwa kile kinachohitajika ili mtu kushtaki serikali.

Muungano huo pia unataka tamko kuwa serikali ya kaunti na maafisa wake wanakiuka wajibu wao wa kisheria kama inavyoagizwa chini ya Sheria ya Mashauri ya Serikali.

Pia inaitaka mahakama kuweka muda ambao pesa hizo zinafaa kulipwa.


Source link

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -spot_img

Most Popular

Home
News
RSS