Thursday, March 2, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsGharama ya maisha yakeketa raia – Ripoti – Taifa Leo

Gharama ya maisha yakeketa raia – Ripoti – Taifa Leo

Gharama ya maisha yakeketa raia – Ripoti

Gharama ya maisha yakeketa raia – Ripoti

NA WANDERI KAMAU

ZAIDI ya thuluthi mbili ya Wakenya inaamini kuwa nchi inaelekea vibaya, imeeleza ripoti iliyotolewa Jumanne na shirika la utafiti la Infotrak.

Ripoti hiyo ilisema kuwa asilimia 62 ya Wakenya wanaamini nchi inaelekea vibaya, asilimia 22 wakisema ina mwelekeo mzuri huku asilimia 15 wakiwa wamegawanyika.

Kulingana na ripoti hiyo, gharama ya juu ya maisha ndiyo iliyotajwa kuwa sababu kuu inayochangia mwelekeo mbaya wa nchi, kwa karibu robo tatu (asilimia 72).

Masuala mengine yaliyotajwa kuchangia mwelekeo huo ni kiwango cha juu cha ushuru (asilimia tano), ukosefu wa ajira (asilimia tano), uongozi mbaya (asilimia nne), siasa mbaya (asilimia tatu) kati ya mengine. Masuala yaliyotajwa kuwatia hofu Wakenya ni gharama ya juu ya maisha (asilimia 72), kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira (asilimia 25), kiwango cha elimu (asilimia 25), kilimo (asilimia 19), ukosefu wa usalama (asilimia 14) miongoni mwa mengine.

Ripoti hiyo ilitolewa huku serikali ikiendelea kujipata katika njiapanda kutokana na malalamishi ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi kuhusu gharama ya juu ya maisha, hasa kupanda kwa bei za bidhaa za matumizi ya msingi kama vile unga wa mahindi, mkate, mafuta ya kupikia na mafuta ya magari kama petroli.

Wakenya wamekuwa wakilalamika kuwa serikali ya Kenya Kwanza haijatimiza ahadi ya kurahisisha gharama ya maisha, licha kutangaza “kuweka mikakati kabambe ya kupunguza bei za bidhaa za msingi”.

Hapo jana Jumanne, wadadisi wa masuala ya uchumi walisema mwelekeo huo ni hali inayofaa kuifungua macho serikali.

“Ikizingatiwa hii bado ni serikali changa, mwelekeo huu si wa kuridhisha hata kidogo. Ni hali inayoonyesha kiwango cha matumaini kwa idadi kubwa ya raia bado kiko chini,” akasema mwanauchumi Tony Watima kwenye mahojiano.

Majuzi, Rais Ruto alisema amefanikiwa kulainisha uchumi, hivyo Wakenya hawapaswi kuwa na wasiwasi hata kidogo.

“Jukumu langu la kwanza katika miezi mitano iliyopita limekuwa ni kulainisha uchumi, kwani ulikuwa umeharibika kutokana na mtindo wa ukopaji na utoaji ruzuku usiofaa,” akasema Rais Ruto alipohutubu wakati wa uzinduzi wa Taifa Fuel katika Kaunti ya Mombasa wiki iliyopita.

Hata hivyo, wale waliosema nchi ina mwelekeo mzuri walitaja hali ya amani iliyopo, utangamano miongoni mwa wananchi, mshikamano wa kiutendakazi baina ya wizara za serikali, gharama ya chini ya maisha kama baadhi ya sababu zilizochangia hali hiyo.

Kuhusu utendakazi wa wizara tofauti, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) iliibukia kuwa bora, kwa kuzoa asilimia 54. Wizara hiyo inaongozwa na Eliud Owalo.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki, alitajwa kuwa waziri bora zaidi, akifuatwa na mawaziri Ezekiel Machogu (Elimu), Ababu Namwamba (Michezo) na Susan Wafula (Afya).

Ripoti ilitolewa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Infotrak, Bi Angela Ambitho.