
JUNGU KUU: Hivi urafiki wa Kenya na China umekatika?
MZOZO ambao umeibuka kuhusu kituo tata cha kibiashara cha China Sq. kilicho katika Chuo Kikuu cha Kenyatta katika Kaunti ya Kiambu, ni moja ya athari za uamuzi wa serikali ya Rais William Ruto kuanza urafiki na mataifa ya Magharibi.
Tangu alipochukua mamlaka Septemba 2022, Rais Ruto amekuwa akiendesha juhudi za kufufua urafiki baina ya Kenya na mataifa ya Magharibi kama vile Amerika na Uingereza, ambao ulidorora kutokana na ukaribu ambao umekuwepo baina ya Kenya na China.
Urafiki baina ya Kenya na nchi za Magharibi ulidorora kuanzia 2003, baada ya Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki kuelekeza mwegemeo wa Kenya kiuchumi na kisiasa katika nchi za Mashariki kama China.
Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alifuata nyayo za Mzee Kibaki, kwa kukuza urafiki baina ya mataifa hayo mawili, hasa kupitia mikopo na miradi tofauti ya maendeleo ambayo imekuwa ikiendeshwa na taifa hilo.
Hata hivyo, Rais Ruto ameonyesha mwelekeo tofauti, kwani ameonekana kuilaumu China kutokana na deni kubwa la kitaifa linaloikabili Kenya.
Katika majukwaa kadhaa, Rais Ruto amenukuliwa akisema ukopaji usio kipimo ndio umechangia Kenya kukumbwa na baadhi ya matatizo ya kiuchumi yanayoiandama kwa sasa.
Hadi sasa, Kenya inakisiwa kuwa na deni la kitaifa la karibu Sh10 trilioni, ambapo kiwango hicho kikubwa kimechangiwa na mikopo ambayo Kenya imekuwa ikichukua kutoka kwa China.
Kutokana na mwelekeo huo mpya wa serikali ya Rais Ruto, wadadisi wanataja hali inayoshuhudiwa katika kituo hicho kuwa “mwanzo tu wa mambo mengi yatakayotokea Kenya inapoelekeza mipango na mikakati yake kiuchumi katika nchi za Magharibi”.
“Mzozo wa China Sq. ni mwanzo tu wa matukio mengi yatakayoshuhudiwa katika siku zijazo Kenya inapoelekeza mikakati yake ya kiuchumi katika mataifa ya magharibi. Huu ni mwanzo tu,” asema Dkt Barrack Muluka, ambaye ni mchanganuzi wa siasa na mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa.
Kulingana naye, licha ya Kenya kufaidika pakubwa kutokana na mikopo ya China, urafiki huo pia umewaathiri sana wafanyabiashara wa kiwango cha chini humu nchini, akitaja hilo kuwa sababu ya wafanyabiashara kutoka eneo la Nyamakima kufanya maandamano jijini Nairobi Jumanne.
“Mojawapo ya matokeo ya urafiki baina ya Kenya na China ni uwepo wa bidhaa za bei rahisi, hali ambayo imewaathiri sana mamilioni ya wafanyabiashara wa kiwango cha chini. Kama hilo halitoshi, sasa Wachina wenyewe wameanza biashara zao nchini (kama vile kituo cha China Sq.), hali ambayo imewaghadhabisha sana Wakenya. Wengi wanahisi kama China ‘imewavamia’ hadi katika makazi yao, ndipo tunaposhuhudia maandamano hayo,” akasema Dkt Muluka.
Wadadisi wanasema kuwa kile kinachoashiria urejeo wa urafiki baina ya Kenya na mataifa ya magharibi ni ziara ambazo Rais Ruto alifanya katika nchi za Uingereza na Amerika mara tu baada ya kuchaguliwa.
Pili, dalili hiyo ni hatua ya Rais Ruto kukubali kutekeleza baadhi ya masharti aliyopewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia kuhusu upunguzaji wa matumizi ya bajeti.
Wadadisi wanasema kuwa ingawa huenda kufungwa kwa kituo hicho kukaonekana kama agizo tu la kawaida lililotolewa na Waziri wa Biashara, Moses Kuria, kuna masuala mengi ya kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi yaliyofichika kuhusu mustakabali wa uhusiano baina ya Kenya na China.
“Kimsingi, huu ni mwanzo wa mwisho kuhusu urafiki baina ya Kenya na China,” asema mdadisi wa siasa Oscar Plato.
Source link