
Hospitali ya Gertrude’s kuandaa matembezi ya hamasisho la saratani
NA LAWRENCE ONGARO
HOSPITALI ya watoto ya Gertrude’s imetangaza kwamba itaandaa matembezi ya kuchangisha Sh15 milioni za kutumika kukabiliana na maradhi ya saratani hasa kwa watoto.
Matembezi hayo yamepangwa kufanyika mnamo Mei 21, 2023 na dhamira iko katika kusaidia watoto kutoka kwenye familia za kipato cha chini wapate matibabu.
Matembezi hayo yataanza kàtika bustani ya Uhuru Gardens jijini Nairobi na ni ya mwendo wa umbali wa kilomita 13 kufika eneo la barabara ya Southern Bypass.
Mkurugenzi katika Hospitali hiyo Dkt Robert Nyarango amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika matembezi hayo ili kufanikisha mipango hiyo ya kuwajali watoto wasio na uwezo wa kupata matibabu.
“Watoto wengi wanapambana na maradhi ya saratani lakini ugonjwa huo hugunduliwa dakika za mwisho ikiwa umepita kiwango chake,” akasema Dkt Nyarango.
Aliongeza kwamba asilimia 80 ya maradhi ya saratani huweza kutibiwa lakini mtoto mmoja kati ya kumi hutibiwa saratani hapa nchini.
Mkurugenzi huyo alitoa hakikisho kuwa Gertrude’s ni hospitali iliyojitolea mhanga kutibu watoto wengi wanaogundulika kuugua saratani.
Alisema mafanikio hayo yanahitaji fedha za kutosha na ushirikiano mkubwa kutoka kwa washikadau.
Afisa mkuu wa matibabu Dkt Thomas Ngwiri alisema hospitali hiyo imebuni mbinu ya kukagua watoto walio na saratani na kuwatibu huku pia wakifanyiwa uchunguzi zaidi kiafya.
“Lengo letu kuu ni kuona ya kwamba tunatibu watoto wapatao 1000 wanaugua saratani kwa muda wa miaka mitano ijayo,” alifafanua Dkt Ngwiri.
Hospitali hiyo huweza kuhudumia wagonjwa wapatao 400,000 kutoka matawi 17 nje na jijini Nairobi.
Source link