
JAMVI LA SIASA: ‘Jeshi’ la Uhuru lililobaki Mlimani lafagiliwa lote
NA WANDERI KAMAU
WAANDANI wachache wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta waliokuwa wamebaki katika ngome yake ya Mlima Kenya sasa wameanza kufurushwa kutoka ukanda huo, kutokana na mvutano unaoendelea katika chama cha Jubilee.
Rais Kenyatta ndiye kiongozi wa Jubilee, alichoanzisha na Rais William Ruto mnamo 2013, wakati huo akiwa Naibu Rais.Wawili hao waliunganisha vyama vyao vya The Nationwide Alliance (TNA) na United Republican Occasion (URP) mapema mwishoni mwa 2012 na kubuni Muungano wa Jubilee.
Baadaye, waliunganisha zaidi ya vyama kumi 2017 na kubuni Chama cha Jubilee (JP).
Kutokana na mvutano unaoendelea baina ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Jeremiah Kioni na wabunge ‘waasi’ wakiongozwa na mbunge Kanini Kega wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Sabina Chege (Mbunge Maalum) kati ya wengine, wadadisi wanasema kuwa mwelekeo huo ni ishara ya kufurushwa kwa ‘mabaki’ ya washirika wa Uhuru katika ukanda wa Mlima Kenya.
Bw Kioni anamlaumu Rais William Ruto kwa ‘kufadhili’ mapinduzi ya kisiasa katika chama hicho kupitia mrengo wa Bw Kega.
Hata hivyo, mrengo wa Bw Kega unamlaumu Bw Kioni kwa “kukiuka maamuzi kuhusu mwelekeo wa chama” kwa kushiriki mikutano ya kisiasa ya mrengo wa Azimio la Umoja.Mnamo Alhamisi, Bw Kioni alipata afueni ya muda baada ya Jopo la Kutatua Mizozo katika Vyama vya Kisiasa (PPDT) kusimamisha kwa muda uamuzi wa kumfurusha kama Katibu Mkuu wa chama.
Uamuzi ulikuwa umeidhinishwa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) baada ya kuwasilishwa kwake na Baraza Kuu la Chama (NEC) kuwafurusha uongozini Bw Kioni, Bw David Murathe Kama Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa na Mwekahazina wa Kitaifa Kagwe Gichohi.
Badala yake, mrengo wa Bw Kega ulimteua (yeye) kama Kaimu Katibu Mkuu, mbunge Adan Keynan (Eldas) kama Kaimu Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa na mbunge Rachael Nyamai (Kitui) kama Mwekahazina wa Kitaifa.
Wadadisi wanasema kuwa uwepo mzozo huo ni dalili za kuondolewa kwa waandani wachache wa Bw Kenyatta waliobaki katika eneo la Mlima Kenya.
“Kabla ya mzozo huo kuibuka, Bw Kenyatta alikuwa na matumaini kuwa waandani wake kama Bw Kega na Bi Chege wangemsaidia kurejesha na kufufua ushawishi wake katika ukanda wa Mlima Kenya. Hata hivyo, mwelekeo wao kuunga kuanza kuunga mkono mrengo wa Kenya Kwanza wake Rais Ruto ni ishara wazi kuwa waandani wa Bw Kenyatta wameanza kupungua kabisa katika ngome yake,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Kulingana naye, matumaini yaliyokuwepo ya Bw Kenyatta kurejesha usemi wake katika Mlima Kenya umevurugika kabisa.
“Jubilee ndicho chombo halisi ambacho Bw Kenyatta angetumia kurejesha usemi wake. Alikuwa na nafasi kukijenga upya na kukipamba chama hicho kama chama halisi cha ukanda wa Mlima Kenya. Hata hivyo, ‘mapinduzi’ yanayoendelea yanaashiria dalili za mwisho za chama na yeye binafsi kama kiongozi wa kisiasa,” akasema Bw Mutai.
Wadadisi wanasema kuwa ‘kifo’ cha kisiasa cha Bw Kenyatta kinajiri wakati ashatangaza mikakati ya kutojiondoa katika siasa licha ya kustaafu kama rais.
Bw Kenyatta alitoa kauli hiyo wiki iliyopita katika Kaunti ya Siaya, baada ya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha.
“Ikiwa mrengo wa Bw Kega utafaulu kumfurusha Bw Kioni nje ya Jubilee, hilo litakuwa sawa na kumkata miguu kabisa kisiasa Bw Kenyatta na matumaini yote yaliyokuwepo kurejesha usemi wake katika Mlima Kenya,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mdadisi wa siasa.
TAHARIRI: Raila ajifunze kudumisha washirika wake kisiasa
Source link