
Jurgen Klinsmann aajiriwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Korea Kusini
Na MASHIRIKA
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani na Amerika, Jurgen Klinsmann, 58, ameteuliwa kuwa mkufunzi mpya wa timu ya taifa ya Korea Kusini.
Klinsmann aliyesaidia Ujerumani kutwaa Kombe la Dunia mnamo 1990 akiwa mchezaji, sasa atadhibiti mikoba ya Korea Kusini kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu ijayo.
Anatarajiwa kuongoza Korea Kusini kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa kwa pamoja na Canada, Mexico na Amerika mnamo 2026.
Hata hivyo, mechi yake ya kwanza kambini mwa kikosi hicho ni pambano la kirafiki dhidi ya Colombia jijini Ulsan mnamo Machi 24, 2023.
Klinsmann alifunga mabao 47 kutokana na mechi 108 alizochezea Ujerumani. Anatua kambini mwa Korea Kusini kujaza pengo la kocha Paulo Bento aliyejiuzulu baada ya kikosi chake kuaga fainali za Kombe la Dunia 2022 katika hatua ya 16-bora nchini Qatar.
Klinsmann ni mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspur. Alijiuzulu kuwa kocha wa Hertha Berlin ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) zaidi ya miaka mitatu iliyopita baada ya kuhudumu kwa wiki 10 pekee.
Chini ya ukufunzi wake, wenyeji Ujerumani waliambulia nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2006 na aliwahi kuongoza Amerika hadi raundi ya muondoano kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2014 nchini Brazil.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
Source link