
Kanisa lakosoa vikali mahakama kwa uamuzi tata kuhusu mashoga
NA BENSON MATHEKA
UAMUZI wa Mahakama ya Upeo ulioruhusu mashoga nchini kuwa na shirika lao unaendelea kuzua joto huku viongozi wa kidini wakiukosoa vikali na kuutaja kama tishio kwa maadili na jamii.
Mnamo Ijumaa, Mahakama ya Upeo ilitupilia mbali rufaa ambayo serikali ilipinga kusajiliwa kwa shirika na makundi ya kutetea mashoga na wasagaji ikisema wana haki ya kuwa na shirika la makundi yao kama Wakenya wengine.
Hata hivyo, viongozi wa kidini wamejitokeza kukashifu uamuzi wa korti huku baadhi wakitishia kuandamana kuulaani wakisema ni sawa na kuruhusu jamii kukumbatia dhambi.
Kulingana na chama cha Wataalamu Wakristo Kenya (KCPF), uamuzi wa korti unaenda kinyume na katiba inayotambua uhusiano wa kimapenzi wa watu wa jinsia tofauti.
“Uamuzi huo unafungua njia ya kusambaratisha nguzo zetu za kisheria, maadili na utamaduni dhidi ya tabia ya ushoga inayoharibu watu binafsi, familia, jamii na nchi,” chama hicho kilisema kwenye taarifa.
Wataalamu hao walisema kuwa ingawa katika uamuzi wake korti haikuondoa sheria zinazopinga ushoga, iliashiria kuwa mashoga na wasagaji wanaweza kushiriki vitendo vyao na kwa kufanya hivyo, majaji walibomoa vizuizi vya kisheria dhidi ya mapenzi kati ya watu wa jinsia moja.
Nao wahubiri wa Kiislamu walikashifu uamuzi huo na kutangaza kuwa wataandamana ili kuokoa vizazi vya Kenya visiangamizwe na ulawiti. Wahubiri hao wamealika Wakenya kwa maandamano ya kukashifu uamuzi huo mnamo Machi 17.
Askofu Wycliffe Nyaperah wa kanisa la Legio Maria alitaja uamuzi wa kuruhusu mashoga kusajili shirika lao lisilo la kiserikali kama kinyume na mafundisho ya Ukristo.
“Kulingana na maadili ya Kikristo katika Biblia, ngono inafaa kuwa ya kuendeleza kizazi na sio kwa sababu nyingine yoyote ile. Ni ya watu waliooana wa jinsia tofauti na sio wa jinsia moja,” alisema Askofu Nyaperah katika taarifa kwa vyombo vya habari na akiongeza kuwa kanisa hilo linahimiza Wakenya wanaothamini maadili na umuhimu wa familia katika kuendeleza vizazi kupinga uamuzi wa Mahakama ya Upeo wa kuhalalisha ushoga.
Majaji Philomena Mwilu, Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u walisema kwamba ni kinyume cha katiba kuzima haki za kuungana, kwa kukataa kusajili chama, kwa kutegemea msimamo wa mtu wa kingono.
Source link