
VITUKO: Kweli kipendacho roho ya Jesus ni Raiane pekee!
IMEKUSANYWA NA CHRIS ADUNGO
NYOTA wa Arsenal, Gabriel Jesus, amerudiana na kidosho Raiane Lima na kudokezea mashabiki kuwa harusi iko njiani.
Jesus, 25, alifichua hayo wiki hii, siku chache baada ya mwanamitindo maarufu wa Croatia, Ivana Knoll, kuanika penzi lake kwa sogora huyo raia wa Brazil.
Jesus na Raiane, 22, walitemana kwa muda mfupi mwezi uliopita na kisura huyo akafuta kwenye Instagram picha zote alizowahi kupigwa akiwa na dume lake.
Hata hivyo, walionekana wakiponda raha wiki hii huku Raiane amevalia pete kubwa ya almasi.
Alikiri kuwa ni “zawadi maridhawa kutoka kwa mume mtarajiwa kadri tunavyojiandaa kula yamini ya ndoa”.
Mbali na picha hizo wakisisimuana kwa mahaba jijini London, Uingereza, Jesus alipakia mitandaoni video ya safari yake ya hivi karibuni nchini Brazil akiwa na Raiane pamoja na mtoto wao wa kike, Helena, mwenye umri wa miezi minane.
Jesus, ambaye amefungia Arsenal mabao matano katika mechi 14, amekuwa mkekani tangu ajeruhiwe goti akitumikia Brazil dhidi ya Cameroon katika Kombe la Dunia nchini Qatar mwezi Desemba.
Kabla kuanza kumtambalia Raiane kimapenzi, Jesus alikuwa akilidokoa tunda la kidege Ludimilla Oliveira naye Raiane alikuwa akimlisha asali Rodrigo Novaes.
Source link