
Mabaharia saba kubeba msalaba wa mlanguzi
NA WAANDISHI WETU
MABAHARIA waliopatikana na hatia ya ulanguzi wa mihadarati ya Sh1.3 bilioni iliyopatikana kwenye meli Mombasa miaka tisa iliyopita, wako hatarini kufungwa jela maisha huku wahusika halisi wakikosa kujulikana.
Wiki iliyopita, Mahakama ya Mombasa iliwapata raia hao saba wa kigeni na hatia ya kusafirisha tarkiban kilo 400 za heroini ambazo baadhi zilikuwa zimechanganywa ndani ya mafuta.
Hakimu Mkuu Martha Mutuku, alisema Yousuf Yakoob, Yakoob Ibrahim, Saleem Muhammad, Bhatti Abdul Ghafour, Baksh Moula, Pak Abdolghaffer na Muhammed Saleh, walishindwa kujitetea wala hawakusema walikuwa wametumwa na nani kusafirisha mizigo hiyo haramu.
Wakenya watatu ambao ni Mohamed Osman Ahmed, Khalid Agil and Maur Bwanamaka, waliondolewa mashtaka baada ya mahakama kubainisha kuwa walikuwa tu madalali wala hawakulipwa kwa kazi waliyofanyia meli hiyo.
Washtakiwa hao saba leo Jumatano wanatarajiwa kujitetea mahakamani, kabla ya hukumu yao kutolewa. Upande wa mashtaka uliomba saba hao wapewe hukumu ya maisha jela.
Kisa hicho cha ulanguzi kiligonga vichwa vya habari kimataifa, baada ya aliyekuwa rais, Bw Uhuru Kenyatta, kuagiza na kusimamia ulipuaji wa meli ya Mv Amin Darya iliyofahamika pia kama Al Noor, ndani ya Bahari Hindi, Mombasa mwaka wa 2014.
Ingawa washtakiwa hawakutaja mahakamani walikuwa wakisafirisha mizigo hiyo kwa niaba ya nani, baadhi ya mashirika ya kimataifa yalimhusisha mfanyabiashara wa Dubai na biashara hiyo haramu.
Jopo maalumu la kuangazia hali ya Somalia na Eritrea katika Baraza la Kiusalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), lilitoa ripoti mnamo 2015 likisema kuwa uchunguzi wake ulibainisha kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na mabaharia waliokuwa kwenye meli husika.
Ripoti hiyo pia iliibua uwezekano wa mfanyabiashara huyo ambaye hatuwezi kumtaja kwa sababu za kisheria, anashukiwa pia kuwa na uraia wa Iran na inaaminika alikuwa akishirikiana na kundi la kigaidi la al-Shabaab nchini Somalia.
“Katika uchunguzi kuhusu ufadhili wa Al-Shabaab, jopo hili lilipokea habari za kuaminika kuhusu meli ya Mv Amin Darya. Habari zilizopokewa zinaonyesha kuwa meli hiyo ilitia nanga kwa siku 10 katika bahari ya eneo la Hobyo, Somalia ya Kati, kabla kuelekea Kenya,” ikasema ripoti yao.
“Kwa muda huo, meli ilisafirisha bidhaa pamoja na wapiganaji, wanaoaminika kuhusiana na al-Shabaab, ambao baadaye walishuka kwenye meli. Mfanyabiashara wa Dubai, ambaye pia anaaminika kuhusiana na Al-Shabaab, alikuwa akiwasiliana na walanguzi mara kwa mara,” ikaendelea kueleza.
Hata hivyo, jopo hilo liliongeza kuwa kuna uwezekano pia meli hiyo ilikuwa ikifanya biashara nyingine za magendo Somalia ambazo hazihusiani na kundi la Al-Shabaab.
Katika uamuzi wake dhidi ya washtakiwa hao saba, Hakimu Mutuku alisema wapelelezi walikusanya na kuhifadhi ushahidi wa kutosha kabla ya meli kulipuliwa na serikali.
Source link