Friday, March 3, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsMajengo ya sasa si kama ya zamani – Taifa Leo

Majengo ya sasa si kama ya zamani – Taifa Leo

Majengo ya sasa si kama ya zamani

Majengo ya sasa si kama ya zamani

NA FARHIYA HUSSEIN

ENEO la Majengo katika Kaunti ya Mombasa miaka kumi ya nyuma lilifahamika kuwa ni kitovu cha uhalifu kwa sababu vijana wengi walipata mafunzo ya itikadi kali ya kigaidi.

Eneo hilo lilipata sifa mbaya kwa kuleta mafunzo yenye itikadi kali ya kigaidi kwa vijana iliochangia wengi wao kujiunga na kundi la al-Shabaab nchini Somalia.

Ni hapa pia ambapo wahubiri wawili wa Kiisalmu waliuawa, Sheikh Aboud Rogo na mwenzake Sheikh Abubakar Shariff almaarufu Makaburi. Wawili hao walifahamika kama wahubiri na walikuwa na ufuasi mkubwa.

Wawili hao waliuawa kufuatia uhusiano wao na shughuli zinazohusiana na ugaidi na athari yao ilidhihirishwa na idadi ya vijana waliomiminika kwenye mahubiri yao katika misikiti ya Musa na Sakina. Kwa kiasi fulani sehemu hizo zilikuwa maarufu kwa vijana wengi waliokosa ajira.

Masjid Musa ni msikiti maarufu ulioko Majengo katika Kaunti ya Mombasa. PICHA | WACHIRA MWANGI

Baada ya mauaji ya viongozi wao Sheikh Rogo na Makaburi, baadhi ya vijana walibadilisha Masjid Musa na kuuita msikiti huo Masjid Shuhadaa kama njia ya kuwaomboleza.

Wahubiri hao wawili pia walifahamika kwa kuzuru Masjid Sakina mara kwa mara.

Vijana hao waliendeleza shughuli zao za mafunzo ya itikadi kali hadi maafisa wa polisi walipovamia msikiti huo na kuwakamata baadhi yao mwaka wa 2014, huku wengine wakikimbia na hadi sasa, wameorodheshwa miongoni mwa magaidi wanaosakwa duniani.

Miongoni mwao ni Ramadhan Hamisi Kufungwa, Issa Abdalla Ahmed maarufu Issa Kauni, Ahmed Omar Mentioned maarufu Dogo Tabibu, na Abdullahi Bulati almaarufu Abdullahi Banati.

Hivi majuzi, Idara ya Upelelezi wa Jinai Nchini (DCI) ilitangaza kuwa vijana hao wana silaha huku ikitoa wito kwa umma kutoa taarifa zozote kuhusu waliko ili kusaidia kukamatwa kwao.

Baadaye uongozi wa msikiti huo ulirejelea jina lake la awali la Masjid Musa.

Taifa Leo ilipozuru eneo la Majengo hivi majuzi, wakazi walionekana huru na wenye furaha, wageni nao wakikaribishwa katika vitongoji huku wafanyabiashara nao wakipata uhuru wa kuendesha biashara zao.

Mwanamke apanga nyanya na bidhaa nyingine muhimu za kuuza eneo la Majengo katika Kaunti ya Mombasa mnamo Februari 27, 2023. PICHA | WACHIRA MWANGI

Kulingana na Kaimu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Bw Ronald Mwiwawi, ushirikiano kati ya makundi ya kutetea haki za binadamu, mashirika ya kijamii, viongozi wa kidini na mamlaka za usalama umesaidia kuregesha hali tulivu katika eneo la Majengo.

“Hapo awali vijana hawakushirikishwa katika kufanya maamuzi muhimu. Lakini siku hizi wanahusishwa katika majadiliano haya. Wanapozingatiwa na kupewa nafasi ya kueleza masuala yao, wanajiona kuwa watu muhimu katika jamii,” akasema Bw Mwiwawi.

Aliongezea kuwa semina za mjadala wa amani na warsha zinazoendeshwa na mashirika ya kijamii na mashirika ya haki za binadamu pia zimechangia kwa kuwashirikisha vijana wengi.

“Katika warsha hizo, vijana hupewa ushauri na wenzao ambao wamekuwa mabalozi wa kueneza amani. Pia, wanatolewa mafunzo dhidi ya kujiunga na vikundi vya kigaidi. Machifu na manaibu wao walioajiriwa ni vijana wenzao, hii imesaidia baadhi yao kuwa na uwazi na kuzungumza na maafisa wa serikali kuhusu matatizo yao ya kijamii,” alisema Bw Mwiwawi.

Bw Mwiwawi anaomba serikali ya kitaifa na za kaunti kuandaa programu zaidi akitoa mfano wa Kazi Mtaani, ambayo anabainisha iliajiri vijana kadhaa na kuwasaidia kujiepusha na dawa za kulevya na uhalifu.

Kwa upande wake, Afisa wa Dharura Haki Africa – shirika la kutetea haki za binadamu – Bw Mathias Shipeta anasifu mabadiliko ya eneo hilo, akibainisha kuwa pia yamesababisha kupungua kwa idadi ya kesi za ukosefu wa usalama.

“Tulikuwa baadhi ya waathirika kutokana na yaliyozuka katika eneo hilo. Nakumbuka kuna nyakati nyingine usiku nilikuwa nikizuru vyumba vya kuhifadhia maiti kusaidia familia kutafuta jamaa zao. Tulidhulumiwa kama shirika la kutetea haki za binadamu kwa kiwango ambacho akaunti zetu zilifungwa. Kushuhudia sura mpya ya Majengo ya leo si suala dogo,” alisema Bw Shipeta.

Bw Shipeta aliongezea kuwa kupitia shirika hilo, wanatoa mafunzo ya ujuzi wa biashara kwa vijana wa Mombasa ambapo baada ya kukamilisha wanafadhiliwa na pesa za kuanzisha biashara.

Juhudi nyingine ambazo wameshiriki katika kuhakikisha usalama unapewa kipaumbele katika eneo hilo, anasema, ni kuandaa mazungumzo ya jamii kupitia mabaraza ya umma.

“Wale waliorejea kutoka nchi jirani ya Somalia walipoenda kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab, walifuatiliwa na kuuawa. Hili lilizua hofu miongoni mwa vijana wengine na kuanza kujiepusha na vitendo vya uhalifu. Waliogopa kwamba wangepoteza Maisha yao. Shida ilikuwa wengi wao walikuwa hawana ajira na walitaka kupata pesa rahisi, lakini mara tu wanapokimbia na kurudi, wengine wanajifunza kutoka kwao,” alisema Bw Shipeta.

Viongozi wa kidini kwa upande wao wameomba serikali kuwashirikisha zaidi vijana katika nafasi za ajira.

“Serikali inapaswa kukumbuka kuwa wakati mradi wa maendeleo unafanyika katika ukanda wa pwani, asilimia 70 ya wafanyikazi wanapaswa kuwa vijana ndani ya eneo hilo. Hii itasaidia kudhibiti visa vya ukosefu wa usalama,” alisema Mwenyekiti wa Kitaifa wa Baraza la Ushauri la Waislamu Nchini (KEMNAC), Sheikh Juma Ngao.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Baraza la Ushauri la Waislamu Nchini (KEMNAC), Sheikh Juma Ngao. PICHA | WACHIRA MWANGI

Sheikh Abu Qatada alibainisha kuwa vipindi vya mazungumzo kwenye runinga na redio na mahubiri misikitini siku ya Ijumaa kuhusu umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani vimesaidia baadhi ya vijana kujiepusha na vitendo vya uhalifu.

“Vijana wanatakiwa kuwa na ajira, mtu asiye na kazi anaweza kushawishiwa katika uraibu wa dawa za kulevya na uhalifu kwa urahisi, ikilinganishwa na wale ambao wameajiriwa na wana shughuli,” alisema Sheikh Qatada.

Sheikh Abu Qatada akieleza jinsi vijana wa Majengo wamebadilisha mawazo na kujitenga na uhalifu na ugaidi. Ni picha ya Februari 27, 2023. PICHA | WACHIRA MWANGI

Taifa Leo ilipozuru eneo la Majengo, wakazi walikuwa wakiendelea na biashara zao, huku wengi wao wakiwashukuru maafisa wa usalama kwa kurejesha amani katika eneo hilo.

“Siku kama ya Ijumaa miaka 10 iliyopita haikuwa ya kawaida kwetu. Watoto walikuwa wakichukuliwa mapema kutoka shuleni na kila mtu kuingia ndani ya nyumba kufikia saa sita mchana. Wengine ilibidi wahame kutoka eneo la Majengo ili kulinda familia zao. Hata hivyo, leo tuna furaha kwa kuwa tunaweza kuuza bidhaa zetu hadi usiku wa manane,” alisema Bw Salim Riaka, mfanyabiashara.

Anaelezea kabla ya hapo, ilikuwa vigumu kwa mtu yeyote wa nje kuruhusiwa kufanya biashara katika eneo hilo.

Bi Zulfa Buoga, mwakilishi wa vijana eneo bunge la Mvita kupitia afisi ya Seneta wa Kaunti alisema wanasajili vijana katika mipango tofauti ya kuwawezesha kuanzisha biashara zao.

“Kesi za wazazi kulalamika kwamba jamaa zao wametoweka au kuuawa na maafisa wa usalama zimepungua. Hii ni kwa sababu ya programu kama hizo ambazo wamesajiliwa,” alisema Bi Buoga.

Bi Fadhila Mentioned alitoa wito kwa serikali kubuni mipango itakayosaidia vijana kusafiri nje ya nchi kutafuta ajira.