
MIKIMBIO YA SIASA: Malala atafanikisha ajenda fiche ya Ruto?
NA WANDERI KAMAU
JUHUDI za Rais William Ruto kumaliza ushawishi wa vyama tanzu vya kisiasa katika mrengo wa Kenya Kwanza zinaendelea kushika kasi.
Mara hii, ameamua kumtumia aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Bw Cleophas Malala “kupunguza nguvu” ushawishi wa chama cha Amani Nationwide Congress (ANC) katika eneo la Magharibi.
Wiki iliyopita, Bw Malala aliteuliwa kama Katibu Mkuu mpya wa chama cha UDA, kuchukua nafasi ya Bi Veronicah Maina, anayehudumu kama Seneta Maalum.
Ijapokuwa Bw Malala bado ni mwanasiasa mchanga na mwenye uwezo wa kuingiliana na watu, wadadisi wanatilia shaka uzalendo na msimamo wake kisiasa.
Hii ni ikilinganishwa na historia yake fupi ya kisiasa, ambapo amebadilisha misimamo yake katika hali tatanishi.
Mnamo 2017, Bw Malala alichaguliwa kama Seneta wa Kakamega kupitia chama cha ANC, chake Kinara wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi.
Hata hivyo, safari yake ya kisiasa ilianza mnamo 2013, alipochaguliwa kama diwani kwa tiketi ya chama cha ODM kuwakilisha wadi ya Mahiakalo, katika Kaunti ya Kakamega.
Wakati uo huo, aligonga vichwa vya habari kwa kuandika mchezo tata wa kuigiza uitwao “Shackles of Doom” uliolaani mapendeleo katika ugavi wa rasilmali na ukabila.
Mchezo huo uliigizwa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere, ijapokuwa lawama zilizoibuka kuuhusu ziliifanya Wizara ya Elimu kuupiga marufuku.
Kama utata ulivyoibuka katika mchezo huo, ndivyo safari yake ya kisiasa imekuwa ikikumbwa na utata pia.
Kwanza, licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya ANC kama Seneta wa Kakamega 2017, Bw Malala aligeuka kuwa mshirika wa karibu wa chama cha ODM na mtetezi mkubwa wa chama hicho, Raila Odinga.
Kutokana na hilo, alipewa onyo na uongozi wa ANC.
Baadaye, Bw Malala aliondolewa katika nafasi yake kama Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti kutokana na mizozo na mivutano iliyoibuka katika mrengo wa Nasa.
Nafasi yake ilipewa Seneta wa Kilifi, Stewart Madzayo.
Mwelekeo huo “ulimrejesha nyumbani” kwa Bw Mudavadi. Hili pia ni baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa madai ya kufanya mkutano huku akikiuka kanuni zilizokuwa zimewekwa na serikali kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.
Kutokana na utetezi wake mkubwa wa Bw Mudavadi, alipewa tiketi ya ANC kuwania ugavana katika Kaunti ya Kakamega kwenye uchaguzi wa Agosti mwaka uliopita.
Hata hivyo, alishindwa kunyakua nafasi hiyo, baada ya Fernades Barasa wa ODM kutangazwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Swali linaloibuka ni: Je, ana uwezo kuendesha merikebu ya UDA kisiasa?
Kulingana na mchanganuzi wa siasa Martin Andati, Bw Malala ana uwezo mkubwa ila uaminifu wake kisiasa ni wa kutiliwa shaka.
“Nafasi ya Katibu Mkuu katika chama kikubwa kama UDA ni muhimu sana. Hata hivyo, mtihani uliopo kwa Bw Malala ni kuonyesha uaminifu kisiasa. Hii ni ikizingatiwa amewatema Raila na Mudavadi hapo awali. Ataaminika mara hii?” akauliza mdadidi huyo. Anauliza: “Atakuwa mwaminifu kwa Rais Ruto?”
Source link