Saturday, March 4, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsMamia wala mbwa, mizizi kuzima njaa – Taifa Leo

Mamia wala mbwa, mizizi kuzima njaa – Taifa Leo

Mamia wala mbwa, mizizi kuzima njaa

Mamia wala mbwa, mizizi kuzima njaa

NA WAANDISHI WETU

MAELFU ya Wakenya sasa wanahatarisha maisha yao kwa kula vitu vinavyoweza kudhuru afya zao katika harakati za kupambana na makali ya njaa.

Baa la njaa linaendelea kukeketa maeneo mengi kutokana na ukame ambao umedumu kwa muda mrefu huku Wakenya waliotegemea shughuli za kilimo na ufugaji kujikimu wakiendelea kuteseka.

Ili kujinusuru, Wakenya walioathirika wameamua kula vyakula ambavyo kwa kawaida haviliwi na binadamu na mizizi ya miti, baadhi ikiwa ni sumu na imewasababishia mauti au kulazwa hospitali.

Mnamo Jumanne wakazi wa Seisei, Baragoi, Samburu Kaskazini walipigwa na mshangao baada ya makundi ya watoto kumchinja kelebu (mtoto wa mbwa) kisha kuchoma na kuila nyama yake baada ya kulemewa na makali ya njaa.

Kwa mujibu wa chifu wa eneo hilo Tony Lesokoyo, tukio hilo lilitokea wakati watoto hao ambao wana umri wa kati ya miaka minne na minane walimchinja mbwa huyo kisha kumchoma nyama yake. Kijiji hicho kina familia 140 na zaidi ambao wamelemewa na njaa.

“Watoto hao walikuwa nyumbani pekee yao walipoamua kumchinja mbwa huyo ambaye alikuwa wa miezi sita pekee. Walifanya hivyo, baada ya kuwaambia wazazi wao kuwa walikuwa wakisakamwa na makali ya njaa na walihitaji chakula,” akasema Bw Lesokoyo.

Naibu Kamishina wa Samburu Jackson Oloo alithibitisha tukio hilo na akasema kuwa watatu hao hawakuugua baada ya kumla mbwa huyo. Hata hivyo, alionya kuwa suala la njaa si sababu ya kula nyama ya mbwa au vyakula vingine ambavyo kwa kawaida haviliwi na binadamu.

Mnamo Oktoba 2022, Gavana wa Samburu Lati Lelelit alitangaza kuwa wakazi 157,000 na zaidi wanakabiliwa na njaa kutokana na ukame ambao umekuwa ukishuhudiwa.

Wakazi wa kijiji cha Sinatule, Lokesheni ya Chevaywa nao wanaendelea kuomboleza mauti ya watoto wawili ambao walikufa baada ya kula maharagwe sumu ili kukidhi njaa iliyokuwa imewalemea.

Emmanuel Wamalwa, 3 na Gideon Wamalwa, 2 walikufa mnamo Jumapili baada ya kula maharagwe sumu kutokana na kulemewa na njaa.

Watoto wengine 11 ambao pia walikula maharagwe hayo nao walikimbiziwa hadi hospitali ya Webuye ambapo walipewa huduma za kwanza.

Kwa mujibu wa Chifu wa Chevaywa Alex Goricho, waliandaliwa maharagwe hayo na nyanya yao kabla ya kuondoka asubuhi. Nyanya huyo pia alikula maharagwe hayo kabla ya kuondoka na pia yakamdhuru.

“Mtoto mmoja alipatikana amekufa ndani ya nyumba na mwengine akafa alipofikishwa hospitali ya Webuye,” akasema Bw Goricho. Ilibainika kwamba maharagwe hayo yalikuwa ya mti ambao hupandwa ili kumaliza magugu shambani na si maharagwe ya kawaida.

“Lazima kila moja awe na tahadhari. Licha ya ukame ambao unaendelea na kusababisha njaa, wasile chakula chochote ambacho ni sumu ama kinachotokana na mimea ya sumu,” akaongeza.

Kule Lamu, jamii ya Waboni kwenye baadhi ya vijiji vilivyoko msitu wa Boni wamelazimika kula mizizi na matunda ya mwituni kufuatia njaa inayokabili eneo hilo kwa sasa.

Wakazi wa vijiji vya Mangai, Mararani, Milimani na Basuba wanasema kiangazi kinachoendelea kushuhudiwa eneo hilo kimesababisha njaa kuwatafuna. Kwa hivyo, baadhi yao kuingia msituni humo kuchuma matunda na mizizi ili kutumika kama chakula kuepuka maafa.

Bi Halako Guyo aliomba serikali na wahisani kufanya hima na kuwafikishia chakula vijijini mwao, akishikilia kuwa njaa na uhaba wa maji umeathiri hata elimu maeneo yao.

“Watoto wetu wataingiaje madarasani kusoma ilhali wakitafunwa matumbo yao na njaa? Chakula cha msaada kila kinapowasili husalia Kiangwe,” akasema Bi Guyo.

“Hapa Mangai na Mararani tunaambiwa ni vigumu kufikishwa kwa sababu za kiusalama. Tunakula matunda na mizizi ya mwitu tusife,” akaongeza.
Tangu 2015 wakati serikali kuu ilipozindua operesheni ya kuwasaka Al-Shabaab ndani ya msitu wa Boni, wakazi wamekuwa wakizuiliwa kuingia msituni kwa sababu za kiusalama. Wameomba serikali iwaachilie huru waingie msituni ili kujitafutia chakula.

Hali ni hiyo hiyo Ganze, Kilifi ambapo wakazi wanakabiliwa na ukame kiasi kwamba watoto wameacha shule huku wazazi nao wakiomba msaada kutoka kwa serikali ndipo wanusurike mauti kutokana na njaa hiyo.

Kwenye Kaunti ya Kajiado, hali imekuwa mbaya kiasi kwamba wazazi nao wanafululiza shuleni kujiunga na watoto wao kula chakula cha mchana kinachotolewa bure.

Wazazi wengine na wale wakongwe wanapitia wakati mgumu sana baada ya mifugo yao kufa kutokana na ukosefu wa malisho.
Hakuna nyasi na kwa kuwa ni wafugaji wa kuhamahama sasa hawana njia zozote za kujizimbulia riziki.

Katika shule ya Ilbisil, Kajiado ya Kati, Taifa Leo ilikumbana na wazazi wengine wakiwa na umri mkubwa wakipiga foleni na watoto wao ili kupata makande (Githeri) pamoja na maji ya kunywa.

Wengi wao walionekana kulemewa na uchovu baada ya kutembea kwa kilomita kadhaa kufika shuleni humo.

Katika Kaunti ya Narok makundi mawili eneobunge la Narok Kusini yana uhasama mkali wakizozania maji ya mto Naroosura. Wafugaji wanawalaumu wakulima wa nyanya na vitunguu kwa kuyaelekeza maji ya mto huo kwenye mashamba yao na kuwaacha wakulima wakiteseka.

Wakulima hao wanadaiwa kuziba maji hayo yasifikie maeneo ambayo wafugaji huwanywesha maji mifugo yao.

Ripoti za Wachira Mwangi, Kalume Kazungu, Robert Kiplagat Na Florah Koech