Sunday, February 26, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsMatiang’i apuuza mwaliko wa kuandikisha taarifa katika DCI – Taifa Leo

Matiang’i apuuza mwaliko wa kuandikisha taarifa katika DCI – Taifa Leo

Matiang’i apuuza mwaliko wa kuandikisha taarifa katika DCI

Matiang’i apuuza mwaliko wa kuandikisha taarifa katika DCI

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i Ijumaa hakuenda kuandikisha taarifa katika makao makuu ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) akisema hakupokea samanzi yoyote.

“Dkt Matiang’i hakukabidhiwa samanzi yoyote na afisi ya DCI iliyotiwa sahihi na maafisa watatu wa polisi kulingana na sheria akitakiwa afike katika afisi ya DCI kuandikisha taarifa kuhusu uvamizi wa makazi yake mtaani Karen na polisi usiku wa Februari 8/9,2023,” mawakili Paul Macharia, Shadrack Wamboi na Danstan Omari wakathibitisha.

Mabw Macharia, Wamboi na Omari walisema Dkt Matiang’i alisikia tu katika vyombo vya habari kwamba Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) alimtaka afike katika afisi yake kuandika taarifa.

Wakizugumza katika mahakama kuu ya Milimani jana mawakili wa Dkt Matiangi’ walisema hata wao hawakubabidhiwa samanzi kwa niaba ya mteja wao akitakiwa kufika makao makuu ya DCI.

Mabw Macharia, Wamboi na Omari walisema samanzi iliyokuwa inasambazwa katika vyombo vya habari ikidaiwa imepelekewa Dkt Matiang’ii ilikuwa feki na yamkini “ilitayarishiwa River Street.”

Mawakili hao walifafanua kwa mapana na marefu jinsi sheria inavyoelekeza jinsi mmoja anatakiwa kuitwa afike kuandika taarifa kuhusu tukio fulani.

Mabw Macharia, Wamboi na Omari walisema waziri huyo wa zamani hakuenda katika afisi hiyo ya DCI kwa vile “hakujulishwa kirasmi.”

Bw Omari alisema bayana kwamba Dkt Matiang’i haogopi kufika katika afisi za DCI kuandikisha taarifa na kujibu maswali atakayoulizwa kuhusu uvamizi katika makazi yake ya kifahari ya Karen na watu waliodhaniwa kuwa maafisa wa polisi.

Mawakili hao walisema samanzi rasmi kutoka kwa DCI ama kituo chochote cha polisi huwa imetiwa sahihi na maafisa watatu wa polisi.

Mawakili hao walimtaka DCI athibitishe alitoa samanzi rasmi kwa Dkt Matiang’ii akimtaka afike katika afisi yake Ijumaa.

“Nilipotakiwa kufika katika afisi za DCI nilionyesha wanahabari samanzi rasmi niliyopokea kutoka kwa DCI. Samanzi ya Dkt Matiang’ii iwapi?” aliuliza Bw Omari.

Mawakili Danstan Omari (kulia), Shadrack Wamboi (kati) na Paul Macharia wanaomwakilisha waziri wa zamani wa usalama Dkt Fred Matiang’i. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Mawakili hao watatu walifafanua kuwa sheria imeweka wazi utaratibu wa kumataka mmoja kufika katika DCI kuandikisha taarifa.

“Kufikia sasa Dkt Matiang’i hajakabidhiwa samanzi afike DCI. Angelipewa samanzi rasmi angelienda bila kusita,”alisema Bw Wamboi.

Mawakili hao walimlaumu DCI kwa kuwapotosha wanahabari na nchi nzima kwamba Dkt Matiang’ii anatakiwa kufika DCI kuandikisha taarifa Ijumaa.

Mawakili hao walikashfu utendakazi wa mkurugenzi mpya wa DCI Amin Mohamed wakisema “hazingatii sheria na akiendelea kuvunja sheria tutawasilisha kesi atimuliwe kazini.”

Mawakili hao walisema afisi ya DCI imebuniwa kwa mujibu wa sheria na Bw Mohamed aliteuliwa kwa mujibu wa sheria na “lazima afanye kazi kulingana na sheria. Akipotoka na kufanya kazi kiholela hatutakuwa na budi ila kuwasilisha kesi atimuliwe kazi.”

Mawakili hao walisema Mahakama kuu ilimwachilia Dkt Matiang’i kwa dhamana ya Sh200,000 na kuamuru polisi wasimkamate ama kumzuilia katika kituo chochote cha polisi.

Alhamisi wiki hii fisa mkuu wa uchunguzi wa jinai Michael Sang alimtaka waziri huyo wa usalama wa zamani afike afisini mwake kuandika taarifa kuhusu uvamizi wa makazi yake na watu waliodhaniwas kuwa polisi.

Mawakili walisema sheria inamtaka afisa kutoa agizo mmoja aende kuhojiwa lakini Sang hakufanya vile.

“Samanzi halisi kwa mujibu wa Sheria za Idara ya Polisi (NPS) lazima itiwe sahihi na maafisa watatu. Nionyesheni samanzi iliyotiwa sahihi na maafisa watatu wa polisi,” Bw Omari alimtaka Sang athibitishe.

Mahakama kuu ilimwachilia kwa dhamana ya Sh200,000 na kuamuru polisi wasimtie nguvuni.

Jaji Kanyi Kimondo aliwataka polisi watii agizo hilo.