
Gachagua: Matiang’i ni mwoga kupindukia
NA WINNIE ONYANDO
NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anadai aliyekuwa Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i alitorokea Uingereza baada ya kuambiwa aandikishe taarifa katika makao makuu ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI).
Akizungumza Jumamosi, Bw Gachagua alidai kuwa hatua ya Dkt Matiang’i kusafiri inaonyesha uoga.
“Sasa aliambiwa aandikishe taarifa kwa DCI akatoroka. Angekuwa mwanaume kamili angekuwa nchini. Niliwaambia kuwa hawa watu ni waoga,” akasema Bw Gachagua.
Haya yanakuja muda mfupi tu baada ya Bw Gachagua kudai kuwa uoga unamfanya Bw Matiang’i ahisi kuwa anafuatwa.
“Matiang’i anahisi kuwa anafuatwa. Alifikiria kuwa tungewatuma maafisa wa polisi kumuandama alivyotufanyia,” akasema Bw Gachagua.
Haya ni kufuatia siku chache baada ya Idara ya Uhamiaji kutoa taarifa kwa DCI kuhusu safari ya Dkt Matiang’i.
Wiki jana, Dkt Matiang’i hakuenda kuandikisha taarifa katika makao makuu ya DCI akisema hakupokea samanzi yoyote.
“Dkt Matiang’i hakukabidhiwa samanzi yoyote na afisi ya DCI iliyotiwa sahihi na maafisa watatu wa polisi kulingana na sheria akitakiwa afike katika afisi ya DCI kuandikisha taarifa kuhusu uvamizi wa makazi yake mtaani Karen na polisi usiku wa Februari 8/9,2023,” mawakili Paul Macharia, Shadrack Wamboi na Danstan Omari walisema.
Source link