
Messi na Mbappe wabeba PSG dhidi ya Marseille na kuweka rekodi mpya za ufungaji wa mabao
Na MASHIRIKA
LIONEL Messi, 35, alifunga bao lake la 700 akitandaza soka katika ngazi ya klabu na kusaidia waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) kusalia kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) baada ya kutandika Olympique Marseille 3-0 mnamo Jumapili.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Argentina aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili baada ya Cristiano Ronaldo kufikisha idadi hiyo ya mabao katika ligi kuu tano za bara Ulaya; yaani EPL (Uingereza), La Liga (Uhispania), Bundesliga (Ujerumani), Serie A (Italia) na Ligue 1 (Ufaransa).
Mechi kati ya Marseille na PSG ilimpa pia nyota Kylian Mbappe jukwaa la kupachika wavuni mabao mawili na hivyo kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa PSG, kwa pamoja na kigogo Edinson Cavani aliyepachikia miamba hao mabao 200 kabla ya kuyoyomea Valencia mnamo Agosti 2022.
PSG sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama 60, nane zaidi kuliko nambari mbili Marseille ambao pia wametandaza mechi 25.
Mbappe aliwafungulia PSG ukurasa wa mabao katika dakika ya 25 baada ya kumegewa krosi na Messi aliyecheka na nyavu katika dakika ya 25 kabla ya kutoa krosi nyingine iliyojazwa kimiani na Mbappe mwanzoni mwa kipindi cha pili.
Mbappe, 24, alihitaji chini ya mechi 250 zilizosakatwa na Cavani kuwa mfungaji bora wa muda wote wa PSG waliomsajili kutoka AS Monaco ya Ufaransa mnamo 2017.
Kwa upande wake, Messi sasa amefunga mabao 28 tangu abanduke Barcelona na kuingia katika sajili rasmi ya PSG mnamo Disemba 2022.
Akiwa miongoni mwa wachezaji bora wa muda wote duniani, Messi alipachika wavuni mabao 672 kutokana na mechi 778 alizosakatia Barcelona walioanza kujivunia maarifa yake akiwa na umri wa miaka 13.
Nyota huyo ameshinda sasa mataji saba ya Ballon d’Or na kunyanyua mataji 35 tofauti akichezea Barcelona na mengine mawili akivalia jezi za PSG. Anatarajiwa kutawazwa Mchezaji Bora wa Fifa 2022 mnamo Februari 27, 2023.
Ronaldo alivuka idadi ya mabao 700 kutokana na mechi za ngazi ya ligi mwanzoni mwa msimu huu wa 2022-23 akichezea Manchester United kisha akahamia Al Nassr ya Saudi Arabia akijivunia mabao 701 katika soka ya klabu za bara Ulaya.
Messi pia ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Argentina (magoli 98) na anakaribia kuwa mchezaji wa tatu kuwahi kufunga mabao 100 akivalia jezi za mabingwa hao mara tatu wa Kombe la Dunia.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
Source link