
SHINA LA UHAI: Mradi walenga kuokoa wanawake ukiangazia HIV, kansa
NA PAULINE ONGAJI
MIAKA miwili iliyopita Bi Caroline Adhiambo Dede, mkazi wa kijiji cha Mariwa, Kaunti ya Homa Bay, kama kawaida alizuru hospitali ya wilaya ya Ogongo ili kupokea dawa zake za kupambana na makali ya HIV (ARVs).
Alipofika huko hata hivyo, Bi Adhiambo ambaye aligundulika kuwa na virusi vya HIV mwaka wa 2005, hakujua kwamba pia angegundulika kuugua kansa ya lango la uzazi kwani hakuwa na ishara zozote.
“Katika harakati za kupokea dawa zangu, nilihimizwa kufanyiwa uchunguzi wa pap smear ambapo matokeo yalithibitisha kwamba nilikuwa kwenye awamu ya kansa ya lango la uzazi ambapo daktari aliamuru nianze kupokea matibabu mara moja,” aeleza.
Baadaye Bi Adhiambo alianza matibabu ya brachytherapy (utaratibu unaotumika kutibu baadhi ya kansa na maradhi mengine)katika hospitali moja ya kibinafsi eneo la Mbita.
“Matibabu hayo yalikuwa ya awamu tatu kwa miezi mitatu,” aongeza.
Hata hivyo, asema kwamba baada ya kukamilisha awamu zote tatu za matibabu hayo, bado hakupata nafuu na hivyo alilazimika kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Homa Bay, huku sampuli zake zikichukuliwa na kusafirishwa hadi Nairobi kwa uchunguzi zaidi.
“Nililazwa hospitalini kwa wiki mbili. Baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani, matokeo ya uchunguzi wa sampuli zilizokuwa zimechukuliwa, yalirejeshwa ambapo daktari alinihakikishia kwamba hali yangu ilikuwa imeimarika, na tokea hapo nikaanza kutumia dawa za kila mwezi.”
Mwezi Agosti 2022 alihakikishiwa kwamba kansa ilikuwa imetoweka, japo kwa sasa angali anaendelea kupokea matibabu ya ziada.
Bi Adhiambo ni mmoja wa wanaofaidika na mradi wa kuunganisha matibabu dhidi ya virusi vya HIV na upimaji kansa ya lango la uzazi, chini ya shirika la Vukisha 95, ambao umekuwa ukitekelezwa katika Kaunti ya Homa Bay.
Mradi huu ulianzishwa Oktoba 2020 ambapo ulilenga wanawake kati ya umri wa miaka 25-49 kutoka kaunti hii.“Tulichagua Kaunti ya Homa Bay kutokana na sababu kuwa ni mojawapo ya kaunti zinazokumbwa na mzigo mkubwa wa virusi vya HIV,” aeleza Bi Alaska Wattoyi, Afisa wa kiufundi katika mradi huo.
Utaratibu wa mpango huu unahusisha wanawake wanaoishi na virusi vya HIV kupimwa dhidi ya maradhi ya kansa ya lango la uzazi wanapokuja hospitalini kupokea dawa zao za ARVs.
“Wale wanaopatikana na kansa ya lango la uzazi, kando na kupokea dawa zao za ARV, wanaelekezwa kwa uchunguzi zaidi ambapo matibabu yatatolewa kuambatana na awamu ya kansa waliyo nayo,” aeleza Bi Wattoyi.
Kuanzia Oktoba 2020 zaidi ya wanawake 26,000 walipimwa kansa ya lango la uzazi huku wanaoishi na virusi vya HIV wakinufaika zaidi.
“Asilimia 56 ya wateja wanaoishi na virusi vya HIV walikuwa wakipimwa kila mwaka ikilinganishwa na asilimia 14 pekee ya wateja ambao hawakuwa na virusi vya HIV.”
Kulingana na Dkt Jacob Khaoya, kiongozi mkuu wa huduma za kimatibabu katika shirika la Vukisha 95 na mtaalam wa huduma za matibabu dhidi ya virusi vya HIV, kuunganisha shughuli za kupima kansa ya lango la uzazi na matibabu ya virusi vya HIV ni muhimu.
“Hii ni hasa ikizingatiwa kuwa wanawake walio na virusi vya HIV wanakumbwa na hatari ya kuathiriwa na kansa ya lango la uzazi mara sita zaidi wakilinganishwa na wale ambao hawana virusi hivi.”
Dkt Khaoya asisitiza kwamba utambuzi wa mapema wa kansa ya lango la uzazi hasa kwa wale wanaoishi na virusi vya HIV husaidia wagonjwa kuanza kupokea matibabu mapema na kukabili maradhi haya kabla mgonjwa hajalemewa.
Kulingana na Dkt Catherine Nyongesa, mtaalamu wa matibabu ya kansa jijini Nairobi,kansa ya lango la uzazi ni mojawapo ya aina za saratani hatari sana na zilizokithiri miongoni mwa wanawake.
“Kwa bahati mbaya, hakuna ishara za mapema za maradhi haya, na pindi mgonjwa anapoanza kushuhudia ishara, maradhi haya huwa tayari yamesambaa.”
Takwimu zinaonyesha kwamba hapa nchini ni asilimia ndogo ya wanawake wanaogundulika kuwa na kansa ya lango la uzazi mapema na kufanyiwa matibabu kabla ya mambo kuwa mabaya.
Njia bora ya kudhibiti maradhi haya, Dkt Nyongesa asema, ni kufanya utambuzi wa mapema ambao hasa hufanywa kupitia uchunguzi wa pap smear unaosaidia madaktari kugundua vidonda au seli zisizo za kawaida kwenye lango la uzazi, na ambazo zaweza tibiwa kabla ya kugeuka na kuwa na uwezo wa kusababisha kansa.
“Tatizo ni kwamba wanawake wengi huenda hospitalini wakiwa wamechelewa ambapo mara nyingi kansa hii huwa imeenea katika sehemu zingine, na hivyo kufanya iwe ngumu kupokea matibabu na kuokoa maisha ya mgonjwa,” aeleza.
Kulingana na mtaalam huyu, kupimwa ndio mbinu ya kutambua maradhi haya kwani yaweza saidia kuzuia aina nyingi za kansa ya lango la uzazi kwa kutambua mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye seli za lango la uzazi ili ziweze kutibiwa.
Source link