
Muungano maarufu KEWOPA wazindua kampeni ya kuvumisha mavazi yanayotengenezwa nchini
NA CHARLES WASONGA
WABUNGE wanawake wameanzisha kampeni inayolenga kuwapiga jeki watengenezaji nguo wa humu nchini na mavazi ya kiasili wanayotengeneza.
Chini ya mwavuli wa Chama cha Wabunge na Maseneta wa Kike Nchini (KEWOPA) viongozi hao Jumanne walisema kuwa kampeni hiyo itaendelea kwa muda wa wiki moja.
Katika muda huo, viongozi hao watakuwa wakivalia mavazi yaliyosanifiwa na kushonwa na mafundi wa nguo wa humu nchini kama njia ya kuhimiza Wakenya kununua mavazi hayo.
“Wanachama wa KEWOPA wanalenga kuvumisha biashara hizi za usafinishaji na ushonaji wa nguo za humu nchini. Kampeni hii inalenga kupiga jeki viwanda vidogo vya humu nchini vya kutengeneza nguo kwa kuwatia Wakenya shime kununua nguo zao,” Seneta maalum Veronica Maina akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Jumanne, Februari 21, 2023.
Viongozi hao walisema waliamua kuanzisha kampeni hiyo kutokana na mchango mkubwa ambao biashara ndogo (SMEs) huchangia katika uzalishaji wa nafasi za ajira, uzalishaji mali, juhudi za kupunguza umasikini na uzalishaji wa mapato.
“Kwa hivyo, tunawahimiza Wakenya kuungana nasi katika kampeni hii yenye malengo mazuri ya kuinua wasanifishaji na washonaji mavazi ya nchini,” Bi Maina akahimiza.
Mbunge Mwakilishi wa Kilifi Getrude Mbeu alisema kuwa tayari anaendeleza kampeni hiyo kwa kuwasaidia jumla ya washonaji nguo 120 katika eneo bunge la Malindi.
“Kwa mfano wiki iliyopita, niliwanunulia cherahani kadhaa pamoja na mahitaji mengine ili waweze kupanua biashara zao. Hata vazi hili ambalo nimevaa limesanifiwa na kushonwa na mmoja wa mafundi hao,” akasema.

Mbunge Maalum Irene Mayaka alisema watu walioko uongozini wanafaa kuongoza katika juhudi za kusaidia viwanda vya humu nchini kwa kununua bidhaa zao na kuwahimiza Wakenya kuiga mfano huo.
“Kama viongozi sharti tuhakikisha kuwa biashara za humu nchini zinanawiri. Njia moja ya kufanya hivyo ni kununua bidhaa zao,” akasema Mbunge huyo aliteuliwa na chama cha ODM.
Mbunge wa Naivasha Jane Kihara alisema inasikitisha kuwa vijana wengi siku hizi huwa hawasomei kozi ya ushonaji nguo kwa sababu watu wengi hupenda kununua mavazi yaliyotengenezwa ng’ambo na kuingizwa nchini. Aidha, akasema, wengine wao huamua kununua nguo kuukuu, almaarufu mitumba.
“Kozi za ushonaji nguo zimefifia kwa sababu watu wengi huwa hawanunua mavazi yao kutoka kwa mafundi wa humu nchini. Sharti tuwasaidie mafundi wa nguo wa kule vijiji kwa kununua mavazi wanayotengenezwa humu nchini,” akasema Bi Kihara.
Mbunge huyo alisema kununua mavazi yaliyotengenezwa na kushonwa nchini kunaweza kuchangia juhudi za kufufua uchumi wa nchi hii unaoyumbayumba.

KEWOPA ni muungano wa wabunge na maseneta wa kike kutoka vyama vyote vya kisiasa vinavyowakilishwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti; waliochaguliwa na walioteuliwa.
Muungano huu unalenga kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nyanja zote za maisha, kuwapa uwezo wanawake ili waweze kushiriki katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Source link