Sunday, March 5, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeUncategorizedMwili wa sogora Christian Atsu wapatikana chini ya vifusi vya nyumba yake...

Mwili wa sogora Christian Atsu wapatikana chini ya vifusi vya nyumba yake nchini Uturuki – Taifa Leo

Mwili wa sogora Christian Atsu wapatikana chini ya vifusi vya nyumba yake nchini Uturuki

Mwili wa sogora Christian Atsu wapatikana chini ya vifusi vya nyumba yake nchini Uturuki

Na MASHIRIKA

MWANASOKA Christian Atsu amepatikana akiwa ameaga dunia chini ya vifusi vya nyumba yake wiki mbili baada ya tetemeko kubwa la ardhi kufanyika nchini Uturuki na kusababisha zaidi ya vifo 40,000.

Sogora huyo raia wa Ghana ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 31, aliwahi kuchezea vikosi vya Everton, Chelsea na Newcastle United katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Atsu hakuwa amepatikana tangu Februari 6, 2023 lilipoporomosha nyumba yake katika eneo la Antakya, Hatay, Uturuki.

“Hakuna maneno yanayotosha kuelezea huzuni yetu. Hatutakusahau. Amani iwe nawe,” ikasema sehemu ya taarifa ya klabu ya Hatayspor iliyokuwa kijivunia huduma za Atsu.

Baada ya tetemeko hilo la ardhi kutokea, Hatayspor iliripoti kuwa Atsu alikuwa ameokolewa kwenye vifusi vya nyumba yake huku akiwa na “majeraha mabaya”. Hata hivyo, msimamo huo wa kikosi hicho ulibadilika siku chache baadaye.

Nana Sechere ambaye ni wakala wa Atsu jijini Hatay, alithibitisha kifo cha mteja wake mnamo Jumamosi kupitia mtandao wa Twitter.

“Kwa huzuni kubwa, nawatangazia kwamba mwili w Christian Atsu umepatikana leo asubuhi. Pole zangu zifikie familia na wapendwa wote ambao wameguswa na msiba huu,” akasema.

Shirikisho la Soka la Ghana limesema mwili wa Atsu ulipatikana baada ya “wiki mbili za mahangaiko na mateso ya hisia”.

Mwili wa Atsu tayari umesafirishwa hadi nchini Ghana kwa mazishi. Atsu alijiunga na Hatayspor mnamo Septemba 2022 baada ya kuchezea Al-Raed ya Saudi Arabia kwa msimu mmoja. Alifunga bao la ushindi katika mechi ya Ligi Kuu ya Uturuki (Tremendous Lig) mnamo Februari 5, 2023.

Hadi kuaga kwake, alikuwa amechezea Black Stars mara 65 na kusaidia timu hiyo ya taifa ya Ghana kutinga fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2015 ambapo walizidiwa maarifa na Ivory Coast kupitia penalti. Atsu aliibuka mchezaji bora zaidi wa kipute hicho.

Alijiunga na Chelsea kutoka FC Porto ya Ureno mnamo 2013 na akachezea klabu kadhaa kwa mkopo ikiwemo Everton na Bournemouth.

Aliwahi kuongoza Newcastle kupanda ngazi kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship) hadi EPL mnamo 2016 na akasajiliwa kabisa na kikosi hicho kilicho baada ya mkopo mnamo 2017.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO