
MIZANI YA HOJA: Ni vizuri kutenda wema maishani lakini usitende wema zaidi ya uwezo wako
NA WALLAH BIN WALLAH
KWA hakika tunakubaliana sana na mafunzo ya kidini yasemayo kwamba umpende jirani kama unavyojipenda wewe mwenyewe.
Kumpenda ndugu au jirani ama mtu mwingine ni kitendo cha utu, ubinadamu na uadilifu mkubwa zaidi katika kuendeleza maisha mema.
Lakini tusisahau funzo au fumbo muhimu lililomo ndani ya wasia huu. Tunaambiwa umpende jirani au ndugu au rafiki au mtu yeyote kama unavyojipenda.
Siri kubwa ni kwamba ujipende wewe mwenyewe kwanza ndipo umpende mwingine. Hayo mapenzi uwe nayo wewe binafsi kwa kujipenda ndipo ugawie watu wengine.
Haiwezekani kumpa mtu kitu ambacho wewe huna! Utampa nini? Kutoka wapi? Pia ni vigumu zaidi kutenda wema zaidi ya uwezo wako hata kama unayo roho safi kiasi gani! Binadamu razini hutenda mambo kulingana na uwezo wake kadri Mwenyezi Mungu alivyomjalia.
Falsafa adhimu katika mizani ya hoja leo ni kwamba, tenda mambo kulingana na uwezo wako. Ishi maisha yanayowiana na kulingana na uwezo wako. Usijibandikie uwezo usiokuwa nao.
Wala usijibebeshe sifa ambazo wewe huna. Kumbuka wa moja havai mbili! Kila mbuzi hula kulingana na urefu wa kamba yake! Sifa za bandia na uwezo wa kujibandika ni mizigo ya aibu maishani!
Ukweli mwingine ni kwamba, watu wenye tabia za kuwashinikiza wenzao kuwasaidia tu hata kama hawana uwezo, nao pia wakome! Usimlazimishe mtu akusaidie tu zaidi ya uwezo wake. Hapana!
Source link