
Otondi kufanyiwa matambiko ya Waluo kabla ya kuzikwa Jumamosi
NA RUSHDIE OUDIA
ALIYEKUWA mwenyekiti wa baraza la jamii ya Waluo Willis Otondi atafanyiwa tambiko maalum leo kabla ya kuzikwa Jumamosi.
Matambiko hayo yatafanywa kulingana na utamaduni wa jamii ya Waluo ambao umeandikwa katika kitabu cha Mtamaduni Paul Mboya ‘Luo Kitgi gi Timbegi’.
Katika kitabu hicho, kuna sehemu inayofafanua ibada zinazofanywa wakati mzee anapokufa.
Kabla ya kuzikwa, wazee wataongoza jamii, familia na marafiki katika hafla ya ibada za kitamaduni zitakazohakikisha maisha ya mwenyekiti huyo yanasherehekewa kwa kufuata utamaduni wa jamii ya Waluo.
Taratibu hizo za kitamaduni pia zilitekelezwa Alhamisi wakati mwili wa kiongozi huyo mashuhuri ulipowasili katika Uwanja wa Michezo wa Jaramogi Oginga Odinga katikati ya jiji la Kisumu ili kutazamwa na umma.
Wazee walisema mwili wa Bw Otondi utasafirishwa kwenda kwake Nyahera jua linapotua.
“Mwili wa Mzee hauruhusiwi kuingia nyumbani kwake mapema. Tutasubiri jua litue ndipo tuupeleke mwili wa mzee nyumbani. Tutafanya hivyo kama njia ya kuendeleza utamaduni wetu,” akasema James Ayaga.
Kulingana na Odungi Randa, mjumbe wa Baraza la Wazee la Waluo, leo asubuhi itatengwa kwa ajili ya sherehe za kitamaduni tu nyumbani kwa Bw Otondi kabla ya kuzikwa Jumamosi.
“Baadhi ya matambiko kama vile Tero Buru yatatekelezwa kabla ya Mzee kuzikwa,” akasema Bw Randa.
Tero Buru ni mojawapo ya matambiko yanayotekelezwa kabla ya mwili wa mzee ama kiongozi mashuhuru kupelekwa kaburini.
Wazee na vijana waliochaguliwa hupeleka makundi ya ng’ombe nyumbani kwa marehemu huku wakizunguka boma hilo.
Wale wanaohusika katika tambiko hili kwa kawaida huvalia mavazi ya kitamaduni ya vita ambayo ni pamoja na ngozi, kofia za mkonge, matawi na viatu maalum.
Baada ya haya, kundi la ng’ombe hupelekwa katika eneo la karibu na maji, hasa mito au ziwa ili kufukuza mapepo ya kifo.
Hili litafanyika kwa umbali wa kilomita 10 kutoka katika makutano ya Kiboswa hadi mahali ambapo jamii ya Waluo ilikuwa ikipambana na Wakalenjin. Haya yatafanywa na wazee pamoja na wacheza densi maarufu wa Kochia- Kagan kutoka Kaunti ya Homa Bay.
Source link