
VITUKO: Pesa si shida kwa Messi! Anunulia kila mchezaji wa Argentina iPhone
IMEKUSANYWA NA CHRIS ADUNGO
LIONEL Messi alitumia kima Sh26.7 milioni kununua iPhone 35 za dhahabu kwa kikosi kizima na wafanyakazi wa timu ya taifa ya Argentina, iliyotwaa Kombe la Dunia nchini Qatar mwezi Desemba.
Nyota huyo wa Paris Saint-Germain (PSG) aliagiza simu hizo za kisasa za asilimia 24 ya dhahabu, na zikapokelewa katika kasri lake jijini Paris, Ufaransa, Jumamosi iliyopita.
Kila moja ilikuwa na jina la mchezaji, nambari ya jezi yake na nembo ya timu ya Argentina.
“Nilitaka kufanya kitu maalumu kushukuru wote waliochangia katika ufanisi wa kunyanyulia Argentina Kombe la Dunia nikiwa nahodha na pia kutawazwa Mchezaji Bora wa fainali,” Messi aliambia wanahabari.
Messi mwenyewe aliwasiliana na mjasiriamali Ben Lyons na wakashirikiana pamoja kubuni muundo wa simu hizo ambazo kocha wa Argentina, Lionel Scaloni, amesema “ni zenye tija na fahari”.
Lyons, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa iDesign Gold, alisema “Messi sio tu mchezaji bora duniani bali pia mteja mwaminifu zaidi.”
Source link