
GWIJI WA WIKI: Peter Ndung’u
NA CHRIS ADUNGO
MWALIMU mwenye mapenzi ya dhati kwa taaluma yake huwa na msukumo wa kutaka kujifunza mambo mapya.
Zaidi ya kuchangamkia masuala yanayofungamana na mtaala, ni mwepesi wa kusoma kutoka kwa vyanzo mbalimbali ili awe chemchemi ya maarifa kwa wanafunzi wanaomtegemea.
Safari ya elimu ni sawa na vidato vya ngazi. Mwanafunzi anastahili kupanda vidato hivyo kwa utaratibu ufaao na kuelekezwa ipasavyo katika kila hatua.
Hivyo, mwalimu anapaswa kuwa na ufahamu mpana unaozidi wa wanafunzi wake.
Kwa mtazamo wa Bw Peter Ndung’u Karanja, mwalimu anastahili kufahamu kiwango cha mahitaji ya kila mwanafunzi, kuwa mnyumbufu katika maandalizi ya vipindi vya somo lake na mbunifu katika uwasilishaji wa anachokifundisha.
“Kuhusisha wanafunzi moja kwa moja katika masomo yanayohitaji ubunifu wa kiteknolojia huwapa fursa ya kufanya mambo kwa kujiamini baada ya kuamshiwa hamu ya kuwa wavumbuzi. Mawanda ya fikira zao hupanuka, uelewa wao huimarika na huanza kuona vitu wanavyofundishwa vikiwa vya kawaida mno,” anasema.
Ndung’u alilelewa katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa Bi Mary Wangui na marehemu Bw John Karanja.
Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Mona, Nakuru (1986-1993) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Molo 220 (1994-1997). Ingawa alitamani kuwa daktari wa meno, alihiari kusomea ualimu (Kiswahili/Historia) katika Chuo Kikuu cha Egerton (1999-2002).
Waliomchochea zaidi kujitosa katika taaluma ya ualimu ni Bw Ngugi na Bw Charles Kiarie waliomfundisha katika shule ya upili. Aliwahi pia kusomea Filosofia na Masuala ya Dini katika Seminari ya Mabanga, Bungoma (2003-2005); na kwa sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Laikipia.
Ndung’u alianza kufundisha katika shule ya upili ya St Joseph’s Minor Seminary Molo mnamo Julai 2007. Alihudumu huko kwa miaka mitano kabla ya kuhamia shule ya Molo 220 (2011-2013).
Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri mnamo Januari 2014 na kumtuma Karima Women, Kaunti ya Nyandarua. Amekuwa Mkuu wa Idara ya Lugha shuleni humo tangu 2017.
Mbali na ualimu, Ndung’u pia ni kocha mzoefu wa mpira wa vikapu na mwandishi stadi wa kazi bunilizi. Insha alizokuwa akizitunga shuleni zilimvunia tuzo za haiba na kumfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake. Kipaji cha uandishi kilichoanza kujikuza ndani yake katika umri mdogo kilipaliliwa zaidi na Bi Susan aliyempokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya msingi.
Makongamano pamoja na mijadala ya kitaaluma redioni, runingani, magazetini na mitandaoni ni majukwaa mengine ambayo Ndung’u hutumia kusambaza maarifa na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti na ufundishaji wa Kiswahili.
Tajriba pevu anayojivunia katika utahini wa Kiswahili umemwezesha kuzuru shule nyingi za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha walimu na kuelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.
Ndung’u anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi wanaotangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.
Anaistahi sana familia yake inayozidi kuiwekea taaluma yake thamani na mshabaha. Kwa pamoja na mkewe, Bi Joyce Wairimu, wamejaliwa watoto watatu – Elsie Wangui, Grace Njoki na Ruth Njeri. Bi Wairimu ni mwalimu wa Kiswahili na somo la Biashara katika shule ya upili ya Marmanet, Kaunti ya Laikipia.
TAMTHILIA: Mtiririko wa matukio katika sehemu 11, Onyesho I
Source link