
Raila kupiga lami baada ya AU kumwonyesha lango
NA BENSON MATHEKA
MUUNGANO wa Afrika (AU), umemvua kiongozi wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga wadhifa wa hadhi kubwa wa Mjumbe wa Maendeleo ya Miundomsingi barani Afrika alioshikilia kwa miaka minne na miezi sita.
Bw Odinga aliteuliwa kuhudumu katika wadhifa huo 2018 baada ya handisheki yake na Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta. Barua ya kumsimamisha kazi Bw Odinga iliandikwa Februari 19 na msimamizi wa Muungano wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, lakini ni jana ambapo ilitolewa kwa umma kupitia Wizara ya Mashauri ya kigeni ya Kenya.
Haikubainika iwapo barua hiyo ambayo nakala yake ilitumwa kwa Ubalozi wa Kenya jijini Addis Ababa, Ethiopia ambako kuna makao makuu ya AU ilipokelewa mapema au jana Alhamisi.
Ingawa baadhi ya wadadisi walihusisha kufutwa kazi kwake na mapambano yake dhidi ya serikali ya Rais William Ruto, Bw Mahamat alimpongeza waziri mkuu huyo wa zamani wa Kenya kwa kuhudumu katika wadhifa huo na kwa mchango wake wa kufanya miundo msingi kupewa kipaumbele katika kufanikisha maendeleo barani.
Duru katika AU ziliambia Taifa Leo kwamba serikali ya Kenya iliomba Bw Odinga apokonywe wadhifa huo katika mkutano wa faragha wa marais wa nchi wanachama wa muungano uliofanyika Ethiopia, siku ambayo barua iliandikwa.
AU pia haikufurahishwa na hatua ya Bw Odinga ya kutotambua serikali ya Rais Ruto ambayo muungano huo unatambua na ulichukulia tamko la kiongozi wa upinzani kama kupindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.
Majukumu ya Bw Odinga yamechukuliwa na shirika la Ushirikiano wa Maendeleo Barani Afrika (NEPAD) ambalo limebadilishwa kuwa Shirika la Maendeleo ya Miundomsingi la Muungano wa Afrika, mojawapo ya sababu ambazo zilifanya kiongozi huyo wa ODM kuvuliwa kazi iliyomfanya kuheshimiwa kote ulimwenguni.
“Mchango wako katika safari hii, Mheshimiwa, umekuwa mkubwa. Niruhusu nieleze shukrani zangu kwa kukubali kuhudumu katika jukumu la kutekekeza ajenda ya miundomsingi ya bara,” alisema Bw Faki kwenye barua yake.
Mnamo Disemba 2022, alizuru Amerika kuungana na rais wa nchi tofauti akiwa amealikikwa kama Mjumbe wa Maendeleo ya Miundomsingi Afrika.
Katika barua yake, Bw Mahamat alimtambua Bw Odinga kama mheshimiwa mara tatu, kuonyesha heshima ambayo kiongozi huyo wa upinzani wa Kenya alitunukiwa akishikilia wadhifa huo.
Alialikwa katika makongomano ya viongozi wa AU na jumuiya za kikanda ambako alitambuliwa na kupatiwa heshima kubwa huku akipokewa kwa misafara ya maafisa wakuu wa serikali, mabalozi na kupatiwa ulinzi katika nchi alizotembelea.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watumiaji Bidhaa Kenya, Bw Stephem Mutoro, “kufutwa kazi kwa Bw Odinga kulijiri siku moja baada ya kutangaza kuanza maandamano ndani ya siku 14” na kwamba, AU ilikuwa katika “hali tete na serikali ya Kenya.”
Wadhifa wa Bw Odinga kama mjumbe wa AU, ulikuwa wa kusaidia muungano huo wa Afrika kuharakisha kuungana kupitia miundomsingi, ili kuinua ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.
Alipoteuliwa, alitwikwa jukumu la kusaidia mipango ya NEPAD ya kuinua kujitolea kwa nchi za Afrika kuanzisha na kutekeleza miradi ya miundomsingi.
Jana Alhamisi, Bw Odinga alisema kwamba, kuvuliwa wadhifa huo kutamwezesha kuhusika na majukumu mengine na akaashiria kwamba alikuwa ameomba kujiondoa katika kazi ya AU wiki tatu zilizopita.
“Tulipokutana pembezoni mwa kongamano la pili la Ufadhili wa Miundomsingi Afrika, Dakar, Senegal yapata wiki tatu zilizopita, nilikueleza changamoto za kuendelea kwangu kuwa Mjumbe wa Maendeleo ya Miundomsingi Afrika,” Bw Odinga alisema.
“Kwa muktadha huu,” akaeleza, ninakubali hatua yako ya haraka ya kuniachilia kuendelea na masuala mengine muhimu na ya dharura,” alisema Bw Odinga kwenye barua aliyoandikia Bw Mahamat jana Alhamisi.
Hata hivyo, hakutuma nakala kwa ubalozi wa Kenya jijini Addis Ababa, alivyofanya Bw Mahamat ishara kwamba huenda hatua ya AU ilitokana na presha kutoka kwa Serikali ya Kenya.
Hatua yake inajiri wakati waziri mkuu huyo wa zamani amezidisha mapambano dhidi ya Serikali ya Rais William Ruto ambaye amekataa kumtambua kama rais wa Kenya akidai uchaguzi wa urais wa Agosti 9 ulikumbwa na udanganyifu.
Baadhi ya viongozi wa muungano tawala wa Kenya Kwanza wamekuwa wakishinikiza apokonywe wadhifa huo, hatua ambayo walionekana kuchangamkia.
Hata hivyo washirika wa Bw Odinga walimtetea huku seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi akisema kiongozi huyo wa ODM “aliomba aache kazi hiyo.”
Mbali na kukosa marupurupu aliyopata akiwa mjumbe wa AU, Bw Odinga atakosa ofisi ya kifahari iliyokuwa na wafanyakazi na watafiti jijini Addis Ababa na heshima aliyopatiwa kote ulimwenguni.
Safari na ulinzi wake akiwa katika ziara rasmi pia zilikuwa zikifadhiliwa na kushughulikiwa na AU lakini baada ya kuvuliwa wadhifa huo, atazikosa pamoja na huduma spesheli katika viwanja vya ndege katika nchi alizotembelea na kualikwa kama mjumbe wa AU.
Source link