
Raila, Uhuru wajipata kwenye uwanja telezi
NA WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wamejipata katika njiapanda ya kisiasa miezi sita baada ya Rais William Ruto uchukua usukani, kwa kuendelea kusalitiwa na baadhi ya wanasiasa waliokuwa washirika wao wakuu.
Ingawa wengi walitarajia wanasiasa hao kuendelea kuwaunga mkono vigogo hao wawili baada ya mrengo wa Kenya Kwanza wake Dkt Ruto kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, wengi wao wamewakaidi na badala yake kutangaza kumuunga Rais Ruto au kujiunga na mrengo huo tawala.
Kufikia sasa, baadhi ya viongozi na wanasiasa ambao wamewaasi vigogo hao ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Kenya (COTU) Bw Francis Atwoli, wabunge Kanini Kega (EALA), Bi Sabina Chege (Mbunge Maalum-Jubilee), Bw Nick Salat, Bw James Ongwae, Bw Francis Kimemia, Bi Sicily Kariuki (aliyehudumu kama Waziri wa Maji), Mbunge Samuel Arama (Nakuru Mjini Magharibi) kati ya wengine wengi.
Katika chama cha Jubilee, Bw Kenyatta anakabiliwa na kibarua kigumu kutatua mvutano unaoendelea baina ya makundi mawili–moja linaloongozwa na Bw Kega na jingine linaloongozwa na Katibu Mkuu, Jeremiah Kioni.
Kundi la Bw Kega linajumuisha wabunge ‘waasi’ ambao wametangaza chama hicho kimejiondoa katika Azimio na kuanzisha ushirikiano mpya na Kenya Kwanza.
Hata hivyo, Bw Kioni anasisitiza kuwa Jubilee bado iko ndani ya Azimio.
Wabunge hao walikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano wa maombi ulioongozwa na Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua katika Kaunti ya Nakuru wiki iliyopita. Kabla ya hapo, walikutana na Rais na Naibu Rais katika Ikulu ya Nairobi.
Kinaya ni kuwa, Bw Kega na Bi Chege walikuwa miongoni mwa viongozi walioandamana na Bw Odinga kwenye kampeni zake za urais katika ukanda wa Mlima Kenya na maeneo mengine nchini.
Katika Kaunti ya Nyandarua, Bi Kariuki na aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo, Francis Kimemia, wametangaza kuanza kuiunga mkono serikali ya Rais Ruto. Wawili hao walikuwa miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano wa Rais Ruto katika eneo la Kipipiri, Desemba 2022.
Katika chama cha ODM, Bw Odinga anakabiliwa na kibarua kigumu kudhibiti uasi kutoka kwa wabunge tisa wanaoonekana kumkaidi.Kinaya ni kuwa, wabunge hao ni miongoni mwa viongozi aliowavumisha kwa wapiga kura katika maeneobunge yao.
Tayari, ODM imeanza mchakato wa kuwachukulia hatua za kinidhamu wabunge hao kwa kwenda Ikulu kukutana na Rais Ruto. Wabunge hao ni Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki) Felix Odiwuor maarufu ‘Jalang’o’ (Lang’ata), Paul Abuor (Rongo), John Owino (Awendo) na Seneta Tom Ojienda (Kisumu).
Ingawa baadhi wameripotiwa kuomba msamaha, Bw Odinga amewaambia kuhama chama hicho ikiwa “hawataki kuwa kwenye safari ya kuikomboa Kenya”.
“Ni afadhali tuwe na watu wachache lakini waaminifu kwenye safari ya ukombozi kuliko kuwa na watu wanaotusaliti. Hao ni wasaliti! Ikiwa wanataka kujiunga na Kenya Kwanza, wako huru kufanya hivyo,” akasema Bw Odinga, alipohutubu Busia Jumapili iliyopita.
Kutokana mwelekeo huo, wadadisi wanasema sababu kuu ya wanasiasa wengi kuwaasi vigogo hao wawili ni kuogopa kujipata kwenye baridi ya kisiasa.
“Kwa baadhi ya wanasiasa, miaka mitano ni muda mrefu sana kukaa nje ya siasa, ndiposa wameamua kufanya kila wawezalo kujaribu kujitafutia nafasi kutoka kwa Rais Ruto. Ni msukumo unaotokana na maslahi yao ya kibinafsi,” asema Profesa Macharia Munene, mchanganuzi wa siasa.
Maswali huku mstaafu akiongezwa kandarasi
Source link