Saturday, March 4, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsRoberto Firmino kuagana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23 –...

Roberto Firmino kuagana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23 – Taifa Leo

Roberto Firmino kuagana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23

Roberto Firmino kuagana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23

Na MASHIRIKA

FOWADI mzoefu raia wa Brazil, Roberto Firmino, ataondoka kambini mwa Liverpool mkataba wake ugani Anfield utakapokamilika rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 amekuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool tangu Juni 2015 aliposajiliwa kutoka Hoffenheim.

Firmino alisaidia Liverpool kushinda taji moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA, EFL Cup na Kombe la Klabu Bingwa Duniani (Membership World Cup).

Kufikia sasa, amechezea Liverpool mara 353 ambapo amefunga mabao 107 na kuchangia magoli mengine 70.

Kocha Jurgen Klopp wa Liverpool amesema alimtaka Firmino kusalia ugani Anfield kwa muda zaidi ila sogora huyo akahiari kuondoka wakati ambapo usimamizi ulikuwa ukijadili kandarasi yake mpya.

Firmino amekosa kuwa tegemeo la Liverpool katika kikosi cha kwanza kutokana na wepesi wake wa kupata majeraha mabaya na pia uwepo wa Diogo Jota, Luis Diaz, Darwin Nunez na Cody Gakpo.

Firmino, ambaye ni kipenzi cha mashabiki wengi wa Liverpool, amekuwa akicheza katikati ya wanasoka Mohamed Salah na Sadio Mane. Hata hivyo, Mane, alijiunga na Bayern Munich ya Ujerumani mwishoni mwa msimu wa 2021-22.

Kwa pamoja, walisaidia Liverpool kutwaa taji la EPL mnamo 2019-20, hiyo ikiwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

Firmino amewajibishwa na Liverpool mara 26 katika mashindano yote ya msimu huu na akafunga mabao tisa huku akichangia manne mengine.

Jeraha lilimweka nje ya kikosi kilichochezea Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar. Kivumbi cha EPL kiliporejelewa baada ya fainali hizo, Firmino bado alikuwa mkekani na aliletwa uwanjani katika kipindi cha pili katika ushindi uliosajiliwa na waajiri wake dhidi ya Everton mnamo Februari 13, 2023.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO