
Sasa Academy yaibua warembo wembe katika voliboli
Na JOHN KIMWERE
TIMU za fani mbalimbali huanzishwa kwa malengo tofauti ikiwamo kunoa talanta za wachezaji chipukizi ili wakomae na kutinga kiwango cha kushiriki mashindano ya kimataifa miaka ya halafu.
Sasa Academy ya mchezo wa voliboli ya wasichana wenye umri wa miaka minane hadi 15 ni akademia iliyoasisiwa mwaka 2018 na Padri Lawrence Kibaara wa Kanisa Katoliki la Soweto, Kayole Nairobi.
Wasichana hawa hufanyia mazoezi kwenye uwanja wa St Joach and Ann Soweto Catholic Church, Kayole Nairobi.
”Sababu ya kuanzisha akademia hii ilikuwa kusaka, kutambua, kukuza na kulea talanta za wachezaji chipukizi,” mwenyekiti na kocha wake ambaye kitaaluma ni mwalimu, John Sakonyi Musungu amesema.
Anaongeza kuwa michezo imeajiri vijana wengi wa kike kwa wa kiume hivyo ni muhimu kunoa talanta za wachezaji chipukizi ili kufahamu mengi wakiwa wadogo.

Anadokeza kuwa kanisa hilo ndilo huwasaidia kuendesha shughuli zao pia likisaidiana na Shirikisho la Voliboli ya Kenya (KVF) Tawi la Nairobi.
Pia bosi wa klabu ya mchezo huo ya Path Blazers, Joseph Richard. Aidha anataja wengine ambao huwapiga jeki kwa vifaa vya kuchezea kama; Mwenyekiti wa KVF Tawi la Nairobi, Moses Mbuthia, naibu mwenyekiti wa kwanza wa KVF, Charles Nyaberi, Moses Kimani kati ya wengine.
Kwa jumla anawashukuru kwa msaada wao wa kifedha, vifaa vya kuchezea na ushauri wao pia anatoa wito wazidi kuwaunga mkono maana wanawahitaji zaidi ili kutimiza azma yao kukuza wachezaji na kuibuka wa kutajika miaka ijayo.
”Ninaomba KVF Tawi la Nairobi iwazie kuanzisha ligi za wachezaji chipukizi mitaani ili wengi wapate fursa kunoa talanta zao,” akasema.
Sasa Academy ni mabingwa wa ngarambe ya ISA 2021, ISK 2019 na 2021, Salvon 2019 pia KVF Tawi la Nairobi kwa kitengo cha miaka nane hadi 15.
Mwezi Februari Akademia hiyo iliandaa shindano la Sasa Peace Cup makala ya tatu lililokuwa la wazi ambapo timu hiyo ilibanduliwa kwenye mechi za makundi baada ya kushindwa kufana mbele ya vikosi vya wakomavu.

Ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza ilishirikisha vikosi vya wanaume ambapo timu ya Githurai Kimbo iliibuka mabingwa baada ya kukung’uta Shinners kwa seti 3-1 katika fainali. Kutokana mashindano hayo amegundua kuwa mchezo wa voliboli una mashabiki wengi sawia na soka kwa kuzingatia wengi waliodhuria mechi hizo. Pia amejifunza kuwa wanahitaji mashindano mengi ya aina hiyo mitaani.
Anasema katika akademia hii wanalenga kukuza wachezaji waibuke mahiri kama Jane Wacu, Janet Wanja, Voilet Makuto, Sharon Chepchumba ambaye huchezea klabu ya Aris Thessaloniki nchini Ugiriki.
Kwa ujumla anashauri wachezaji chipukizi nyakati zote waonyeshe nidhamu, wampende na kumtii Mungu, watie bidii darasani na viwanjani, waheshimu wazazi, waalimu na wote wanaowazidi umri.
Kocha huyu anajivunia kufunza voliboli kwenye shule na vyuo vikuu ikiwamo: Kayole South Secondary, Embakasi Girks, Makini College, Huruma Women, Nile Highway Women Secondary na Technical College of Kenya (TUK).
Kwa sasa kando na kufunza Sasa Academy pia hufunza Brownhill Secondary na Chuo Kikuu cha Kimataifa (AIU).
Amehitimu kama kocha wa voliboli daraja la Pili kitaifa(KVF), kiwango cha daraja la Kwanza katika voliboli ya ufukweni barani Afrika (CAVB) pia kimataifa amehitimu kwa kiwango cha daraja la Kwanza (FIVB).
Sasa Academy inajumuisha wachezaji kama: Eisie Janice na Lucy Machel (nahodha na naibu wake), Nelly Wairimu, Pleasure Rose Wanjala, Scholastica Mwende, Mary Christine, Janet Kerubo, Grace Mueni, Getrude Kwamboka, Angel Mueni na Magadeline Wangare.
Pia wapo: Jacinta Syombua, Everlyne Syombua, Juliet Achieng, Sharon Naliaka, Mackline Ajiambo na Cynthia Omusundi.

Source link