
Serikali sasa kutwaa mali ya mshukiwa wa uhalifu
NA BRIAN OCHARO
SERIKALI sasa inataka kuchukua mali za mfanyabiashara, Bw Yusuf Ahmed Swaleh, ambaye alipatikana na hatia ya utakatishaji fedha.
Mali hizo ni pamoja na magari matatu, ambayo serikali inadai yalinunuliwa kwa kutumia mapato ya uhalifu.
“Magari hayo yanaaminika kuwa yalinunuliwa kutokana na fedha zilizopatikana kwa njia ya uhalifu, ambayo ni biashara ya dawa za kulevya na makosa ya utakatishaji fedha,” stakabadhi za serikali zinasema mahakamani.
Upande wa mashtaka unasema kuwa magari matatu yamesajiliwa kwa jina la Bi Asma Abdalla Mohamed, ambaye ni mke wa Bw Swaleh.
Kiongozi wa Mashtaka, Jami Yamina, aliambia mahakama ya Shanzu kwamba serikali itatafuta amri ya kuchukua mali ya mamilioni ya pesa, zikiwemo pesa na magari yanayoaminika kuwa ya uhalifu.
Bw Swaleh na Bi Mohamed tayari walipatikana na hatia kwa kosa la utakatishaji fedha na wanasubiri kuhukumiwa.
Walidaiwa kuwa mnamo Februari 4, 2017 walihusika katika makubaliano ya ununuzi wa magari manne kwa gharama ya Sh7.6 milioni, huku wakijua kuwa fedha hizo zilitokana na uhalifu, ambayo ni biashara ya dawa za kulevya.
Upande wa mashtaka ulisema kuwa madhumuni ya washukiwa kununua magari hayo yalikuwa ni kuficha walivyopata fedha hizo.
Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa walinunua magari mawili ndani ya miezi miwili na kulipa Sh6.2 milioni.Mahakama ilibaini hawakuwa na biashara halali ya kugharimia mamilioni ambayo walikuwa wameweka kwenye akaunti zao, na kuzitumia kununua magari hayo manne.
Aliyekuwa Hakimu Mkuu wa Shanzu, Bi Florence Macharia, alibaini kuwa ingawa walikuwa wameachiliwa katika shtaka la ulanguzi wa dawa za kulevya, walikuwa na jukumu la kuonyesha jinsi pesa zilizotumika kununua magari hayo zilivyopatikana.
Hati zilizowasilishwa mahakamani zinaonyesha kuwa kutokana na taarifa za benki za wanandoa hao, mapato yao ya juu ya mwezi kutoka kwa fomu za kufungua akaunti yalikuwa Sh10,000.
Wanandoa hao walishtakiwa pamoja na Masuo Bakari Tajiri kwa makosa kadhaa ya ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya heroin ya thamani ya Sh47 milioni na utakatishaji fedha.
Hata hivyo, hawakupatikana na hatia kwa shtaka hili, mahakama ikisema nyumba ambayo mali hizo zilipatikana haikuwa yao, na mwenye nyumba hiyo hakushtakiwa.
Bakari aliuawa kabla ya kesi yao kukamilika. Mwili wake uliokuwa umekatwakatwa uligunduliwa kwenye kichaka Thika mwaka 2022, mwezi mmoja baada ya kuripotiwa kutoweka mnamo Desemba 3, 2021.
Chuo chafungwa wanafunzi wakidai kuvamiwa na jini
Source link