Saturday, February 25, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsSerikali ya Ruto ikome kutumia idara za usalama kuwanyamazisha wapinzani – Taifa...

Serikali ya Ruto ikome kutumia idara za usalama kuwanyamazisha wapinzani – Taifa Leo

WANDERI KAMAU: Serikali ya Ruto ikome kutumia idara za usalama kuwanyamazisha wapinzani

WANDERI KAMAU: Serikali ya Ruto ikome kutumia idara za usalama kuwanyamazisha wapinzani

NA WANDERI KAMAU

WAKATI wa harakati wa kupigania Ukombozi wa Pili katika miaka ya 1990, mawakili ni kati ya watu waliohusika katika harakati ya kuukabili utawala wa rais Daniel Moi.

Baadhi ya mawakili hao ni Paul Muite, Gitobu Imanyara, Dkt Gibson Kamau Kuria, Kiraitu Murungi (aliyekuwa gavana wa Meru) kati ya wengine wengi.

Ushiriki wa mawakili katika harakati hiyo ulikuwa muhimu sana kwani waliwasaidia wanaharakati waliokamatwa na vikosi vya usalama kujitetea mahakamani kwa mashtaka waliyofunguliwa na serikali kwa kushiriki katika harakati hizo.

Kama isingalikuwa ushiriki wa mawakili hao, pengine wanaharakati wengi wangejipata pabaya zaidi kuliko hali ilivyokuwa wakati huo. Tangu wakati huo, mawakili wamejidhihirisha kuwa nguzo kuu ya mapambano na harakati za ukombozi wa kisiasa na kiutawala nchini.

Kutokana na hilo, inasikitisha sana wakati serikali inapoonekana kuanza kuwatishia mawakili wanaowatetea watu wanaoipinga au wale wasioiunga mkono.

Hili linafuatia vitisho vya Idara ya Upelelezi (DCI) dhidi ya wakili Danstan Omari, kwa kumwakilisha aliyekuwa Waziri wa Usalama katika serikali iliyopita, Dkt Fred Matiang’i.

Ijapokuwa idara hiyo inasema inamtaka Bw Omari “kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya simu yake”, ni wazi kuwa mwelekeo huu unaashiria lengo la idara hiyo ni kumtishia kwa kumwakilisha Dkt Matiang’i.

Bila shaka, mwelekeo huu ni hatari, kwani unaashiria serikali ya Rais William Ruto imeanza kutumia idara za usalama kuwatishia wapinzani wake.