
Serikali yajikokota kukamilisha ujenzi wa daraja la mbao kisiwani Dongokundu
NA ALEX KALAMA
TAKRIBAN wakazi 500 kutoka kisiwa cha Dogokundu kilichoko katika wadi ya Dabaso, Kaunti ya Kilifi, wanaiomba serikali ya kaunti hiyo kukamilisha mradi wa daraja la mbao ulioanzishwa eneo hilo ili kuwapunguzia changamoto za usafiri.
Wakiongozwa na Kadzo Khoi, wakazi hao wanadai kuwa magogo yaliyowekwa wakati wa ujenzi wa daraja hilo la mbao ambalo halikukamilika, yamezidisha changamoto za usafiri katika barabara hiyo.
“Shida ambayo tunapitia sisi wakazi wa kisiwani ni hii ya njia. Tunaumia sisi akina mama. Watoto wetu wakienda shule tunawabeba; yaani huku umebeba chombo huku umebeba mtoto unampitisha ili aende shuleni. Tuna tabu sana sisi wakazi wa kisiwani kwani ni lazima tutatoka na vidonda kwa sababu ya kukwaruzwa na vitu majini,” alisema Bi Khoi.
Aidha wamesema kuwa hulazimika kutembea takriban kilomita moja huku wanafunzi na wanawake wajawazito wakiaathirika zaidi hasa wakati maji yanapojaa katika njia wanayoitumia.

“Tunaomba kama serikali inatuona au inatusikia tafadhali ituhurumie kwa maana sisi nasi ni wanadamu tunaohitaji maisha ya kupendeza,” alisema Bi Khoi.
Kwa upande wake mwakilishi wa wadi ya Dabaso Emmanuel Changawa ameeleza kusikitishwa na hatua ya kutokamilika kwa daraja hilo la mbao licha ya kutengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2021-2022.
“Kuna mradi wa daraja (Boardwalk) ambao ulikuwa umeanzishwa mwaka wa kifedha wa bajeti 2021-2022 lakini ulikwama. Tunataka umalizwe basi kama kutakuwa na programu nyingine zifanywe baadaye. Wakazi wa hapa wanapata tabu sana… Inakuwa ni shida kwani ili kutembea katika hii barabara inakulazimu uiname baada ya mita mbili mbili hivi katika umbali wa kilomita moja,” akasema Bw Changawa.
Aidha Changawa ameiomba serikali ya kaunti hiyo kuchukua hatua za haraka ili kukamilisha ujenzi wa daraja hilo na kufanya mipango ya kuliboresha daraja hilo siku zijazo.
“Hiki kijiji ni kijiji ambacho kiko na wakazi zaidi ya 500 na hawajafaidi moja kwa moja kutokana na ugatuzi. Kama kiongozi nataka niwaambie wadau kwamba kuna watu kisiwani ambao wanateseka na wanahitaji msaada wa dharura. Kwa hivyo nataka niambie tu serikali ya kaunti huu mradi wa daraja umalizwe basi kama kutakuwa kingine cha kufanywa kifanywe baadaye,” alisema Bw Changawa.
Source link