Monday, February 27, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsThika Queens wawekea Vihiga Queens presha kali ligini KWPL – Taifa Leo

Thika Queens wawekea Vihiga Queens presha kali ligini KWPL – Taifa Leo

Thika Queens wawekea Vihiga Queens presha kali ligini KWPL

Thika Queens wawekea Vihiga Queens presha kali ligini KWPL

LAWRENCE ONGARO Na AREGE RUTH

THIKA Queens FC sasa inafuata Vihiga Queens katika jedwali la Ligi Kuu ya Wanawake Nchini (KWPL) ikiwa na pointi 21 sawa na Gaspo Ladies ambao wako kwenye nafasi ya tatu.

Thika wamepanda baada ya kunyorosha Kayole Starlets mabao 5-0 katika mechi iliyopigiwa uwanjani Thika Stadium.

Kocha Frederick Majani alisema ushindi huo umewaweka pahala pazuri ambapo watafanya juhudi wawe juu bila kuyumbayumba.

“Hatustahili kulaza damu tukidhani eti tumefika hivyo ni vyema sisi tuendelee kufanya bidii,” akasema kocha Majani.

Katika mechi hiyo, wafungaji walikuwa ni Wendy Atieno (3), Sarah Chalovu (1), na Grace Wekesa (1).

Kocha alisema ushindi huo umewapa mwelekeo mwema wa kujipanga kivingine ili kuafikia azma yao.

Aliwapongeza warembo hao kwa kufuata maagizo yake wakati wa mechi hiyo.

“Iwapo vipusa hao watashikilia msimamo huo nina uhakika kuwa tutatawazwa mabingwa wa KWPL ifikapo mwisho wa msimu huu,” akaahidi kocha huyo.

Alisema wikiendi ijayo wanatarajia kupatana na timu ya Zetech ambapo amejiwekea matumaini makubwa ya kupata ushindi.

Mwenyekiti wa kikosi hicho Frederick Chege alisema kikosi chao cha wasichana 22 kipo imara na wanatunzwa vizuri katika makao yao mjini Thika.

“Sisi kama klabu ya kukuza soka ya wasichana tunazingatia pakubwa maslahi yao na ndiyo sababu wamejizatiti kufika mahali hapo,” alisema kinara huyo.

Viungo Janet Moraa Bundi na Sherline Opisa walihakikisha vinara wa KWPL Vihiga Queens wanasalia kileleni mwa jedwali. Hii ni baada ya wawili hao kufunga bao kila mmoja dhidi ya Nakuru Metropolis Queens. Kwa sasa wana jumla ya pointi 22.

Gaspo wako katika nafasi ya tatu baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Wadadia Ladies ugani Gems Cambridge.