
Tulibwagwa, Boga awaaminisha wafuasi wake
NA SIAGO CECE
ALIYEKUWA Katibu wa Wizara ya Kilimo, Prof Hamadi Boga, hatimaye amevunja kimya chake tangu mahakama ilipothibitisha ushindi wa Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani.
Wakazi wawili, Bw Dziwe Zuma na Bw Suleiman Mwanguku, walikuwa wamepinga ushindi wa Bi Achani dhidi ya Prof Boga mahakamani kwa kudai kulikuwa na wizi wa kura. Lakini mahakama ilitupilia mbali madai hayo.
Katika uchaguzi wa ugavana, Bi Achani aliywania kupitia Chama cha UDA alipata kura 59,674 naye Prof Boga akaibuka wa pili akiwa na kura 53,972 kupitia ODM.
Prof Boga, sasa amewaambia wafuasi wake kwamba msimu wa uchaguzi umeisha kwa hivyo waendelee mbele na maisha.
Huku akidokeza kujitolea kusaidia serikali ya kaunti kwa njia yoyote ile, aliomba kusiwe na ubaguzi kwa misingi ya kisiasa kuhusu utoaji huduma kwa wananchi.
Mwanasiasa hiyo alisema masuala kama vile basari na huduma nyingine za kaunti zinafaa kupewa kwa yeyote kwa usawa bila kujali walivyopiga kura.
“Haipaswi kutokea hali ambapo mtu amenyimwa huduma au kutojumuishwa katika shughuli za serikali kwa sababu alikosa kukupigia kura. Mkifanya hivi mtakuwa mmefeli demokrasia. Sina chuki na yeyote. Labda sina mamlaka, lakini nitachangia mawazo ili kuboresha maisha yetu. Tutachangia tuwezavyo hata kama ni kukosoa,” akasema.
Hata hivyo, aliwarai wakazi wa Kwale kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu shughuli za kaunti ili kuwe na uwajibikaji.
Prof Boga, ambaye pia alionekana kudokeza kuwa bado yuko kwenye siasa kwa miaka zijazo, alimtaka Bi Achani awajibike kwa manufaa ya wakazi wa Kwale.
“Wakazi wa Kwale wanatakiwa kuwajibisha viongozi wao walio ofisini, na kuhakikisha kuwa maisha yao yamebadilika na kuwa bora zaidi. Viongozi hawa wana uwezo na rasilimali la kuwezesha jambo hli,” Prof Boga alisema.
Bi Achani hapo awali alisema kuwa yuko tayari kufanya kazi na wapinzani wake wote waliokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2022.
“Tunakaribisha mawazo na hata ukosoaji wao kwa sababu utanifanya kuwa kiongozi bora siku zijazo. Huwezi kujua, ukosoaji wako ndio utanijenga,” Bi Achani alisema katika hafla ya hivi majuzi katika makao makuu ya kaunti.
Mwezi uliopita, Mahakama Kuu iliamua hakuna ushahidi wa kutosha kufutilia mbali ushindi wa Bi Achani, kufuatia kwamba uchaguzi wa ugavana ulikumbwa na dosari.
Wakati Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipomtangaza Bi Achani mshindi wa ugavana, wapinzani wake waliungana na kuashiria kushirikiana kupinga matokeo hayo mahakamani.
Hata hivyo, kesi moja pekee ndiyo iliwasilishwa mahakamani na wapigakura wawili wa Kwale waliotaka matokeo yabatilishwe. Wengine walioshindania kiti hicho ni Bw Chai Lung’anzi na Bw Chirau Mwakwere.
Source link