
Type ni kuoga na kurudi soko, Edday mke wa Samidoh ashauriwa
NA SAMMY WAWERU
EDDAY Nderitu, mke wa kwanza wa mwanamuziki wa nyimbo za Mugithi, Samuel Muchoki maarufu kama Samidoh ameshauriwa ‘kuamka’ na kusukuma gurudumu la maisha licha ya changamoto zinazomzingira.
Ushauri huo umetolewa kufuatia mzozo unaoonekana kulemea ndoa yake na staa huyo, Edday akidokeza kwamba mambo yalianza kuenda mrama miaka mitatu iliyopita.
Mjadala moto umegaragazwa mtandaoni, wachangiaji wakihimiza mama huyo kuchagua kati ya amani na ndoa yenye machozi.
Mjadala huo ulioanzishwa na mwanablogu Martha Mwihaki Hinga aidha umeibua hisia mseto kwenye intaneti.
“Mimi naona tutume Edday kwa Keziah Wa Kariuki. Kuoshwa mchana peupe, kurudi soko, kukosa kujipa tena, kurudi soko kutafutia watoto pesa. Hakuna paragrafu. Ni mwanamke machachari (akimaanisha Keziah),” Mwihaki akaandika katika ukurasa wake wa Fb.
Mwanablogu huyo asiye na picha ya utambuzi, chapisho lake likinuwia kuhamasisha biashara ya Keziah Wa Kariuki, lina ujumbe fiche – Edday awe mwanamke mkakamavu anayejisimamia kimaisha.
Edday awekeze kwenye biashara
Kulingana na maelezo ya utambuzi ya Keziah, ni mwanahabari wa kituo cha runinga cha Kameme (kinachomilikiwa na Shirika la Mediamax) ambaye mbali na kazi yake ya kuajiriwa amewekeza katika biashara.
Huuza bidhaa za wanawake kujirembesha na kujipodoa.
“Kujitafutia pesa, kunakuondolea vikwazo. Keziah Wa Kariuki sasa anatambulika na ana ushawishi. Ana duka eneo la Kahawa Sukari. Wengine hatukuzaliwa tupendwe bwana,” Mwihaki akaelezea kwenye safu ya mchango.
“Ninaomba uende katika duka lake ununue bidhaa anazouza. Mwambie umetumwa na Martha, utapewa na bei iliyopunguzwa.”
Ushauri kwa Edday afanye mahesabu kuhusu maisha yake, umechochea wanamitandao kumhimiza awekeze kwenye biashara badala ya kuletewa kila kitu na mume wake.
Baadhi wamemtaka mama huyo kumlisha Samidoh talaka.
Edday hata hivyo amejibu ushauri aliopewa, akisema anautambua.
“Ninaendelea kuyapokea. Hongera rafiki yangu Keziah Wa Kariuki.”
Dkt Dianah Kamande, mwasisi wa Cometogether Widows and Orphans Group (CTWOO), hata hivyo amemtaka Edday kuwa makini na mseto wa ushauri anaopewa.
Amekosoa hatua yake kuanika masuala ya ndoa yake mitandaoni.
“Achague hekima. Si kila ushauri wa marafiki wanaomzingira utamfaa,” Afisa Mkuu Mtendaji huyo wa shirika linaloangazia wajane na mayatima akaambia Taifa Leo.
“Isitoshe, aainishe mikakati kuwekeza kwenye biashara ajiimarishe. Akiwa mwanamke anayejisimamia, sarakasi tunazosikia katika ndoa yake zitapungua na hata kuisha,” Dkt Kamande akashauri.
Kuchovya asali nje ya ndoa

Siku kadha zilizopita, Edday aliandika katika ukurasa wake rasmi wa Fb ujumbe wa kushangaza akiashiria kuchoshwa na drama za mumewe Samidoh.
Alimlaumu kwa kumkosea heshima pamoja na familia yake.
Samidoh, ambaye pia ni polisi yuko kwenye uhusiano haramu na seneta maalum, Karen Nyamu, wawili hao wakijaaliwa watoto wawili pamoja.
Akimtaja kama kiruka njia, mke wa Samidoh ameonyesha kukerwa na tabia za mume wake kuchovya asali nje ya ndoa.
Samidoh na Edday wana watoto watatu.
Mwanamuziki huyo na Karen wamekiri kuwa wachumba, wakianika paruwanja mitandaoni.
Wawili hao hata hivyo wamekuwa wakizozana mara kwa mara, Desemba 2022 Karen akivamia Samidoh na Edday katika kilabu kimoja Dubai.
Source link