Wednesday, March 1, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsUfugaji bata wanawiri kupitia lishe ya wadudu – Taifa Leo

Ufugaji bata wanawiri kupitia lishe ya wadudu – Taifa Leo

Ufugaji bata wanawiri kupitia lishe ya wadudu

Ufugaji bata wanawiri kupitia lishe ya wadudu

NA LABAAN SHABAAN

UKIINGIA katika shamba la Ololo eneo la Kajiado Kaskazini kilomita 25 kutoka Jiji la Nairobi, utakaribishwa na sauti za bata aina ya white peking baadhi wakilishwa hadharani, wengine wakipumzika chini ya vivuli vya miti huku baadhi yao wakiogelea kwenye mabwawa.

Shambani humu utamkuta Linda Laura ambaye ni mfugaji wa bata takriban 1,000. Wamechagua bata aina ya white peking kwa sababu wana nyama ya thamani ya juu na hutaga mayai vyema. Ololo Farm and Lodge hunadi mazao yao mitandaoni ambapo wateja huagiza mayai na nyama kupitia apu.

Siku za hivi karibuni wafugaji wanaumiza vichwa na gharama ghali ya malisho ya mifugo. Linda anakiri kuwa japo wananawiri katika ufugaji bata, kupata malisho nafuu kibiashara si kupanda mchongoma, ni kushuka hasaa.

“Bata wetu wanakuwa wakubwa ndani ya kipindi kifupi kwa sababu tumeanza mradi wa kufuga wadudu aina ya black soldier flies (BSF) ambao ni chakula cha mifugo. Tunachanganya wadudu hawa na vyakula vingine kupata matokeo bora ya lishe,” Linda anaeleza.

Wadudu wa BSF ambao wako tayari kuliwa na ndege na mifugo. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kadhalika, Linda anaendeleza majaribio ya njia nyingine ya malisho ya bata. Pembezoni mwa sehemu ya kulishia bata, kuna kidimbwi cha kukuzia mimea aina ya azolla. Ni mimea ya naitrojeni inayokuwa kwenye maji na shambani Ololo inatumika kulisha bata.

“Tunabuni mbinu zetu wenyewe kupata vyakula mbadala ili kupunguza gharama ya chakula na kuongeza faida,” anaongeza.

Kevin Getobai, mfugaji wa BSF, anaeleza kuwa wadudu hawa wana uwezo wa kubadilisha mabaki ya chakula na taka kuwa protini. Kwa hivyo wanatokea kuwa chanzo bora cha protini kwa mifugo.

“Hawa viwavi ni chakula cha mifugo na wanatupa mbolea tunayotumia shambani humu Ololo kufanikisha kilimo hai,” Getobai anasema.

Ili kuongeza mapato maradufu, Ololo hufuga bata wengi wa kike zaidi ya kiume. Kwa kila bata watano wa kike, kuna bata mmoja wa kiume kuwezesha kuzaana.

Linda anaambia Akilimali kuwa anapendelea ufugaji wa bata zaidi ya kuku kwa sababu hawaathiriwi na maradhi sana kama kuku akikiri kuwa changamoto kubwa kwa bata ni msimu wa baridi hususan kwa bata wachanga.

Kuepuka hali hii, vifaranga huhifadhiwa ndani ya brooder kwenye joto hadi wawe na manyoya tayari kutolewa nje. Aghalabu utumizi wa dawa za kiasili kama tangawizi, vitunguu saumu na shubiri husaidia Linda kuhakikisha bata wake wana afya nzuri kuvutia soko.

Ololo Farm iko mkabala na Hifadhi ya Wanyama ya Nairobi na ukaribu huu huhatarisha ufugaji kwa sababu wanyama kama fisi na nugu huja usiku, japo mara chache, na kuwala bata.

“Tunachinja na kuuza bata katika Hoteli ya Ololo na wateja wengine mijini hasaa Nairobi kupitia mitandao. Kwa sasa hatuuzi mayai kwa sababu tunayatumia kuangulia vifaranga,” Linda asema.

“Tunauza bata kwa kati ya Sh2,000 na Sh3,000. Pia tunauza nyama kwa kilo kuanzia Sh1,000.

Mayai na nyama ya bata ni bora kwa virutubisho zaidi ya mara tatu ya kuku. Nahimiza wafugaji wajiunge na ufugaji huu,” anaongeza.