Wednesday, March 1, 2023
AdvertismentGoogle search engineGoogle search engine
HomeGeneral NewsValentino ya kifo – Taifa Leo

Valentino ya kifo – Taifa Leo

Valentino ya kifo

Valentino ya kifo

NA TOM MATOKE

ALIYEKUWA mwalimu mkuu wa shule moja ya Msingi katika Kaunti ya Nandi anazuiliwa na polisi kwa madai ya kuhusishwa na mauaji ya kikatili ya mkewe.

Bw Zachariah Ng’asura, ambaye ni mwalimu mstaafu anadaiwa kumuua mkewe Rose Jerono siku ya Valentino kwa kumdunga kwa kifaa chenye ncha kali nyumbani kwao kijijini Chepkumia.

Uchunguzi wa upasuaji maiti, umeonyesha kisa hicho kilichoshangaza wakazi kilitekelezwa usiku wa kuamkia Februari 14.

Kwa muda wa majuma mawili, makachero wataalamu wa masuala ya mauaji kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) wamekuwa wakikita kambi katika eneo la mkasa huo kutegua kitendawili cha ukatili huo.

Wamebaini kwamba mume wa mama huyo na binti yake, walikuwa nyumbani wakati Jerono alikumbana na mauti.

Ripoti ya uchunguzi wa polisi aidha inaashiria Bw Ng’asura ndiye mshukiwa mkuu.

Mkuu wa DCI Kaunti ya Nandi, Douglas Chikanda aliambia Taifa Leo kwamba jamaa huyo huenda ndiye alipanga njama au kutekeleza mauaji ya mke wake, akidokeza kwamba wawili hao wamekuwa wakizozana katika ndoa.

“Aliingia jikoni ambapo mke wake na bintiye walikuwa wamelala, akamdunga kwa kifaa chenye ncha kali, upasuaji wa maiti ukionyesha huenda ikawa alitumia kisu,” Bw Chikanda akasema.

Afisa huyo alisema uchunguzi zaidi unaendelea.

Wawili hao wana watoto sita na inadaiwa mshukiwa alipeleka mkewe hospitalini kupata matibabu ya dharura.

Cha kushangaza kulingana na wanafamilia, jamaa huyo alipita kituo cha afya cha kaunti kilichokuwa karibu na kumpeleka cha kibinafsi mjini Kapasabet, jambo ambalo linaibua maswali.

Hata hivyo, mazishi ya mama huyo yameahirishwa kutokana na ghadhabu ya wanakijiji walioandamana wakiapa kuchukua sheria mikononi dhidi ya mshukiwa.

Naibu spika wa bunge la Nandi, Bw Wilson Sang amehimiza umma kuwa na subira polisi wakamilishe uchunguzi.
Alisema wahusika watakaopatikana na hatia, wataadhibiwa kisheria.