
Vigogo watwaa kazi mahasla wakisubiri tu
NA WANDERI KAMAU
HUKU Rais William Ruto akiendelea kuteua waandani wake katika nyadhifa tofauti serikalini, maswali yameibuka ikiwa atawakumbuka wale wa tabaka la chini maarufu ‘mahasla’.
Hii ni kwa sababu wengi wanaoendelea kutuma maombi ya kazi hizo ni wanasiasa wakongwe waliowahi kuhudumu katika serikali za hapo awali.
Kwenye kampeni zake za urais mwaka 2022, Rais Ruto aliahidi kubuni serikali ya mahasla, itakayowashirikisha watu wa mapato ya chini kama mama mboga, wahudumu wa bodaboda, vinyozi kati ya wengine.
Hata hivyo, mwelekeo ambao umeibuka kufikia sasa ni kuwa, kuna watu maarufu ambao wamekuwa wakituma maombi yao kila nafasi za kazi zinazotangazwa serikalini, hivyo kuonekana kuwanyima nafasi vijana na mahasla.
Baadhi yao ni aliyekuwa gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana, Bi Adelina Mwau (aliyehudumu kama Naibu Gavana wa Makueni), Bw James Ongwae (aliyekuwa gavana wa Kisii), Dkt Evans Kidero (aliyewania ugavana Homa Bay), Bw Charles Njagua (aliyekuwa mbunge wa Starehe), Bw Nicholas Ngumbo (aliyewania ugavana Siaya), Bi Cate Waruguru (aliyehudumu kama Mwakilishi wa Kike, Laikipia), Bi Tabitha Mutemi (anayehudumu katika idara ya mawasiliano katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka –IEBC), aliyekuwa Seneta Maalum Isaac Mwaura, Mbunge Maalum wa zamani Wilson Sossion kati ya wengine.
Baada ya kuhudumu mihula miwili kama gavana wa Makueni, ilitarajiwa kuwa Prof Kibawana, 68, angestaafu kutoka siasani na utumishi wa umma kwa jumla. Hata hivyo, Prof Kibwana ni miongoni mwa watu ambao wametuma barua zao kuomba kazi ya mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Kati ya 1997 na 2002, Prof Kibwana alihudumu kama Msemaji wa Baraza la Kitaifa la Kikatiba (NCEC). Kando na hayo, alihudumu kama mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi kati ya 1977 na 2002. Wakati mmoja, alisimamia kitivo cha sheria katika chuo hicho. Mnamo 2002, alichaguliwa kuwa mbunge wa Makueni, na baadaye akateuliwa Waziri wa Ardhi na Mazingira na Rais Mstaafu Mwai Kibaki. Januari 2008, aliteuliwa kama Mshauri wa masuala ya Kikatiba, Bunge na Vijana katika Afisi ya Rais, nafasi aliyoshikilia hadi Septemba 2012.
Bi Mwau ni miongoni mwa watu wenye ushawishi ambao wametuma maombi ya kuteuliwa Manaibu wa Mawaziri (CASs). Kando na kuhudumu kama naibu gavana wa Makueni, alihudumu kama Mbunge Maalum (2003-2002) wa muungano wa NARC. Pia, alihudumu kama Naibu Waziri wa Leba.
Licha ya kuhudumu kama gavana wa Kisii kwa mihula miwili tangu 2013, Bw Ongwae, 70, ni miongoni mwa wale wametuma ombi la kuteuliwa kama naibu wa waziri. Alianza safari yake katika utumishi wa umma kama mkuu wa tarafa (DO) katika miaka ya sabini, baadaye akawa afisa katika Idara ya Uhamiaji kati ya nyadhifa zingine nyingi. Alipanda ngazi hadi akawa Katibu katika Afisi ya Rais (marehemu Daniel Moi) na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Wafanyakazi (DPM). Aliwahi pia kuhudumu kama Katibu wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) na Katibu katika Wizara ya Kilimo.
Dkt Kidero alihudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Sukari ya Mumias kwa miaka minane na baadaye kama gavana wa Nairobi (2013-2017). Ametuma ombi la kuwa naibu waziri.
Naye Bw Njagua alihudumu kama mkurugenzi katika Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kulevya (NACADA) na baadaye kama mbunge wa Starehe (2017-2022). Anataka kuwa naibu waziri.
Bw Gumbo alihudumu kama mbunge wa Rarieda kati ya 2007 na 2017. Alihudumu pia kama mwenyekiti wa Kamati ya Uhasibu ya Bunge (PAC). Anataka kuteuliwa kama naibu wa waziri.
Bi Waruguru alihudumu kama diwani maalumu katika Bunge la Kaunti ya Laikipia (2013-2017) na baadaye kama Mwakilishi wa Kike (2017-2022). Anataka kuwa naibu waziri.
Kando na kuhudumu katika kitengo cha mawasiliano cha IEBC, Bi Mutemi anahudumu katika Bodi ya Usimamizi ya Baraza la Vyombo vya Habari Kenya (MCK). Alitaka kuwa Katibu wa Wizara japo hakuteuliwa.
Bw Mwaura alihudumu kama Mbunge Maalum (2013-2017) katika ODM na Seneta Maalum (2017-2022) katika Jubilee. Anataka kuwa naibu waziri.
Bw Sossion alihudumu kama Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) na mbunge maalum wa ODM (2017-2022). Anataka kuwa naibu waziri.
Wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakihimiza Rais Ruto atimize ahadi yake ya kuwakumbuka chipukizi badala ya kuwapa kazi watu waliowahi kuhudumu serikalini kwa muda mrefu.
Source link