
Vijana Wapwani wasakwa kimataifa kuhusu ugaidi
NA FARHIYA HUSSEIN
KWA takriban miaka kumi iliyopita, taifa la Kenya limekuwa likijitahidi mno kukabiliana na ugaidi.
Katika juhudi hizo, eneo la Pwani limeibuka kuwa sehemu ambayo imeangaziwa sana kwa idadi kubwa ya vijana ambao hutekwa na itikadi kali za kidini ili wajiunge na makundi ya kigaidi.
Majina ya wahubiri waliokuwa na itikadi kali za kidini kama vile Aboud Rogo na Abubakar Sharif almaarufu kama Makaburi, huibua kumbukumbu za makabiliano makali kati ya polisi na wafuasi wa wawili hao maeneo ya Pwani.
Wawili hao waliuawa kwa kupigwa risasi katika miaka ya 2012 na 2014 mtawalia, baada ya kuhusishwa na uenezaji wa itikadi kali za kidini zilizosemekana kuchochea ugaidi.
Ijapokuwa mashambulio ya kigaidi yamepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya awali, uchunguzi wa Taifa Leo umebainisha kuwa, kuna vijana wengi kutoka Pwani ambao wangali wanatumikia makundi ya kigaidi ama ndani ya nchi au katika mataifa ya kigeni.
Kwa mujibu wa maafisa wa polisi, baadhi ya vijana waliotoweka makwao ghafla washukiwa walienda kujiunga na makundi ya kigaidi nje ya nchi.
Nchi ambazo husemekana vijana hao hutorokea sana ni kama vile Somalia na Msumbiji, ambapo makundi ya kigaidi hupanga njama za kutekeleza mashambulio ndani na nje ya nchi hizo.
Mabw Ramadhan Hamisi Kufungwa, Issa Abdalla Ahmed almaarufu Issa Kauni, Ahmed Omar Mentioned almaarufu Dogo Tabibu, Abdullahi Bulati almaarufu Abdullahi Banati, waalizaliwa na kulelewa katika miji ya Pwani ya Kenya.

Wameorodheshwa na Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), kuwa miongoni mwa washukiwa wa ugaidi wanaosakwa.
Kulingana na DCI, Bw Kufungwa anaongoza wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab na kuratibu mashambulio akiwa Somalia.
Bw Kufungwa amehusishwa na njama ya mwaka wa 2014 ya kuwateka nyara watalii wa kigeni nchini. Anaaminika kuwa kiongozi mkuu wa zamani katika Msikiti wa Masjid Musa, Mombasa, kama wakala mkuu wa uajiri.
Alihusishwa na kuwaajiri Mahir Riziki aliyejitoa uhai na kujilipua katika mkasa wa Dusit, na Bw Mohamed Rashid Mwatsumiro, almaarufu Modi.
Modi aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka wa 2019 baada ya maafisa wa polisi wa Recce kumiminya risasi katika nyumba yake eneo la Ngombeni, Kaunti ya Kwale. Hadi kifo chake, Modi alikuwa mshukiwa wa ugaidi ambaye polisi walimtaja kuwa kiongozi wa genge eneo la Ngombeni.
Ripoti za polisi zilifichua kwamba wawili hao, Modi na Mahir walisafiri hadi Tanzania pamoja, kisha wakaelekea Somalia kujiunga na kundi la al-Shabaab.
Baada ya kufanyiwa mafunzo, ilidaiwa Modi na Mahir walirejea Kenya pamoja ambapo Modi aliunda genge la wahalifu na kuwasajili vijana katika vikundi vya kigaidi Kwale. Mahir alisemekana kupanga kwa usiri kushambulia Nairobi, wakilenga Hoteli ya DusitD2 Januari, 2019.
Inaaminika walikuwa miongoni mwa wengine waliotorokea Somalia baada ya Msikiti wa Masjid Musa kuvamiwa na polisi mwaka wa 2014. Msikiti huo ulihusishwa na kuficha magaidi na silaha.
Watu wengine waliosemekana kuenda Somalia wakati huo ni pamoja na Ahmed Omar Mentioned, almaarufu Dogo, Ramadhan Hamisi Kufungwa, Mohamed Ebrahim almaarufu Daddy, na Salim Ahmed Mohamed almaarufu Lascano, ambao bado hawajakamatwa.
DCI pia imemhusisha Kufungwa na Bw Kassim Musa Mwarusi ambaye maafisa wa upelelezi wamemtaja kuwa aliyehusika na kutekeleza mashambulizi eneo la Boni na kuongoza vikundi vingine vya kigaidi kutoka Kenya.
Kulingana na wataalamu wa masuala ya sheria na usalama, Pwani hulengwa na magaidi kusajili vijana wajiunge nao kwa sababu mbalimbali.
Miongoni mwao ni jinsi ukanda huo una mipaka inayoweza kutumiwa kuingia na kutoka nchini, dhuluma za kihistoria kama vile ukosefu wa ajira na changamoto za raia wa kawiada kumiliki ardhi, na ulanguzi wa dawa za kulevya.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, alisema ukuaji wa teknolojia pia unachangia kukithiri kwa uhalifu wa kimataifa, unaojumuisha pia ulanguzi wa binadamu na dawa za kulevya.
“Ni muhimu kwetu wataalamu wa sheria Afrika kuzidisha juhudi za kukabiliana na uhalifu wa kimataifa. Hii inatuhitaji kuweka mikakati na hatua za kisheria zinazowiana na hali halisi ilivyo barani Afrika,” akasema, katika warsha ya wakurugenzi wa idara za mashtaka barani Afrika iliyofanyika Mombasa hivi majuzi.
Washukiwa wengine wanaosakwa zaidi kutoka miji ya Pwani ni pampoja na Bw Issa Abdalla Ahmed almaarufu Issa Kauni na Bw Ahmed Omar Mentioned almaarufu Dogo Tabibu kutoka Malindi, Kaunti ya Kilifi.
Ahmed anasemekana kujiunga na kundi la al-Shabaab na kusafiri hadi Somalia mwaka wa 2014, anapodaiwa kuwa kwenye kikosi cha magaidi wa kujitoa mhanga.
Mwaka 2022, Rashid Salim Mohamed almaarufu kama Chotara, alikamatwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa njiani kuelekea Afrika Kusini kwa mipango ya ugaidi. Inaaminika kuwa alitoroka Kenya mwaka wa 2019 baada ya kukosa kufika mahakamani Mombasa kwa shtaka linalohusiana na ugaidi.
Mchanganuzi wa masuala ya kiusalama, Bw Elkana Jacob, anahoji kuwa masuala ya ukosefu wa ajira na utumizi wa dawa za kulevya ambayo hayajatatuliwa Pwani, huchangia sana magaidi kupata njia rahisi ya kushawishi vijana eneo hilo kujiunga nao.
Katika mwaka wa 2020, polisi walitaja Kaunti ya Kwale kuwa na sehemu ambazo magaidi wanatumia kama ngome za kuficha magaidi.
Source link