
Wabunge wafuatilia matumizi ya Sh 55B siku za mwisho za Uhuru uongozini
NA CHARLES WASONGA
WABUNGE wameanzisha kuchunguza madai kwamba, Serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ilitumia Sh55 bilioni bila idhini ya bunge miezi miwili kabla ya kiongozi huyo kuondoka mamlakani Septemba 13, 2022.
Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) jana Jumanne ilianza kuchunguza malalamishi hayo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watumiaji Bidhaa Nchini (COFEK) Stephen Mutoro akisema, hatua hiyo ni kinyume na kipengele cha 223 cha Katiba ya sasa.
Kamati hiyo, chini ya uongozi wa Mbunge Maalum John Mbadi inayo muda wa siku 60 kuchunguza malalamishi hayo kabla ya kuwasilisha ripoti yake kwa kikao cha bunge lote.
“Inasikitisha kuwa kiasi hicho kikubwa cha pesa kilitumiwa na serikali kati ya Julai na Septemba, kinyume cha Katiba wakati taifa lilikuwa likizongwa na mzigo mkubwa wa madeni, mfumko wa bei na kupanda kwa gharama ya maisha,” akasema Bw Mutoro kwenye malalamishi yaliyosomwa bungeni mnamo Desemba 6, 2022.
Bw Mutoro sasa anataka Bunge la Kitaifa kuamuru Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu kuchunguza kwa undani matumizi yote ya pesa za umma yaliyofanywa na Serikali ya Kitaifa kati ya Julai na Septemba 13, 2022, Rais William Ruto alipoingia afisini.
Katibu huyo Mkuu wa Cofek anasema amewasilisha pendekezo hilo kwa wabunge baada ya juhudi zake za kutaka malalamishi yake yashughulikiwe na Wizara ya Fedha kugonga mwamba.
“Uchunguzi huo unafaa kufanywa haraka kwa sababu sakata nyingi hufanyika siku chache kuelekea mpito kutoka utawala mmoja hadi mwingine. Ikiwa huu mwenendo wa serikali inayoondoka mamlakani kutumia pesa za nyingi za umma bila idhini ya bunge hautadhibitiwa sasa, utaendelea kushuhudiwa na kuchangia wizi wa pesa za umma,” akaeleza.
Bw Mutoro aliongeza kuwa pesa hizo, Sh55 bilioni, zilitumika ilhali hazikuwa zimetengwa katika bajeti ya kitaifa ya Sh3.3 trilioni.Kulingana na kipengele cha 223, Serikali ya Kitaifa sharti ipate idhini ya Bunge la Kitaifa kabla ya kutumia pesa za umma.
Na endapo Serikali imetumia pesa hizo kwa shughuli za dharura, bunge likiwa likizoni, Waziri wa Fedha anapaswa kusaka idhini hiyo miezi miwili baada ya pesa hizo kutumika.Jana, Bw Mutoro alitarajiwa kufika mbele ya kamati ya PAC, inayoongozwa na Mbunge Maalum John Mbadi kutetea madai yake lakini akafeli kufanya hivyo.
Wabunge walikataa kumsikiza mwalikishi wake wakimtaka Bw Mutoro afike bungeni mwenyewe.
Mnamo Oktoba 2022, Idara ya Bajeti Bungeni (PBO) iliwasilisha ripoti kwa wabunge ikionyesha kuwa, Hazina ya Kitaifa ilisambaza Sh54.68 bilioni kwa matumizi katika Wizara, Idara na Mashirika ya Serikali Kuu (MDAs) bila idhini ya bunge “siku chache kabla muhula wa pili wa Bw Kenyatta kukamilika”.
Kulingana na ripoti hiyo ya PBO, Wizara ya Kawi na Mafuta ilipewa Sh16.6 bilioni za kufadhili ruzuku kwa bei ya mafuta, Wizara ya Miundo Msingi ilipewa Sh11.35 bilioni za ujenzi wa barabara, Wizara ya Elimu ilipewa Sh8.2 bilioni za mpango wa Elimu Bila Malipo katika Shule za Msingi na Upili.
Aidha, Sh6.1 bilioni zilitumwa kwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya kusaidia kampeni ya mawasiliano ya Telkom Kenya, pesa ambayo maelezo kuhusu matumizi yake hayakutolewa.
Wizara ya Kilimo nayo ilipokea Sh4.5 bilioni za kugharimia ruzuku ya bei ya unga wa mahindi huku Sh3.5 bilioni zikielekezwa kwa Wizara ya Ulinzi kufadhili ujenzi wa hospitali ya kuendeshea utafiti.
Maelezo kuhusu matumizi ya Sh3.77 bilioni zilizoelekezwa kwa Afisi ya Rais hayakutolewa.
Source link