
CDF: Wabunge watisha kuangusha bajeti ya ziada
NA CHARLES WASONGA
KWA mara nyingine wabunge wametisha kuzima Bajeti ya Ziada baada ya Hazina ya Kitaifa kuchelewesha kutolewa kwa jumla ya Sh36.28 bilioni pesa za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF).
Wabunge ambao ni wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha zilizogatuliwa wamemsuta Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u kwa kile walichataja ni “kuwachezea shere Wakenya wakati huu mgumu wanapohitaji huduma katika maeneo bunge.”
Wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Gideon Mulyungi, wabunge hao walisema kufikia sasa Hazina ya Kitaifa imetoa Sh10 bilioni pekee ambazo zimetumika kugharamia karo za wanafunzi kutoka familia masikini.
“Hazina ya Kitaifa haijatoa fedha za NG-CDF za kugharimia maendeleo ilhali imesalia miezi minne pekee kabla ya mwaka huu wa kifedha wa 2022/2023 kukamilika. Je, serikali imefilisika au nini kinaendelea?” Bw Mulyungi ambaye ni Mbunge wa Mwingi ya Kati akauliza.
“Tunaitaka serikali itoe Sh34.28 bilioni zilizosalia ili zitumike kufadhili miradi ya maendeleo pamoja na Sh2 bilioni ambazo zilisalia kutokana na mgao wa fedha wa mwaka wa kifedha wa 2021/2022. Ikiwa hatutapata hakikisho kuwa pesa hizo zitatolewa ndani ya mwezi mmoja ujao, basi hakutawa na haja kwetu kupitisha Bajeti ya Ziada itakapowasilishwa bungeni hivyo karibuni,” akasema, kauli ambayo iliungwa na wanachama wengine wa kamati yake.

Wabunge hao walitoa malalamishi hayo Jumanne katika majengo ya bunge, Nairobi, walipokutana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kitaifa ya Hazina ya NG-CDF Yusuf Mbuno. Mkutano huo ulilenga kutathmini taarifa za kifedha za hazina hiyo.
Mbunge wa Kitui Mashambani David Mboni alisema kuwa maeneo bunge yatajipata pabaya kimaendeleo ikiwa mwaka huu wa kifedha utakamilika Juni 30, 2023 kabla ya serikali kuu kutuma pesa zote za mgao wa NG-CDF.
“Tunafaa kutoa ilani kwa Hazina ya Kitaifa kabla ya sisi kupitisha Bajeti ya Ziada. Ikiwa kwa mara nyingine tutakuwa na masalio ya fedha za NG-CDF basi baadhi yetu kama wabunge tutapatwa na wakati mgumu katika maeneo bunge yetu. Huenda wananchi wakatukataa,” Bw Mboni akasema.
Wabunge pia walimsuta Waziri Profesa Ndung’u kwa kupotosha Bunge kwamba Hazina ya Kitaifa itakuwa ikitoa Sh2 bilioni za NG-CDF kila wiki kuanzia Desemba, 2022.
“Mbona waziri anawadanganya wabunge na Wakenya kwamba atakuwa akitoa Sh2 bilioni kila mwaka ilhali kuanzia Desemba 2022 hakuna chochote?” akauliza Mbunge wa Mugirango Magharibi Stephen Mugaka.
Katika mwaka huu wa kifedha wa 2022/2023, Hazina ya NG-CDF ilitengewa Sh44.24 bilioni katika bajeti ya kitaifa iliyosomwa bungeni na aliyekuwa Waziri wa Fedha Ukur Yatani mnamo Aprili 7, 2022.
Akiwajibu wabunge hao, Bw Mbuno alisema kuwa afisi yake imepata hakikisho kutoka kwa Hazina ya Kitaifa kwamba Sh34.28 bilioni za NG-CDF zitatolewa hivi karibuni ili kuyawezesha maeneo bunge kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa.
“Tumepata hakikisho kutoka kwa Hazina ya Kitaifa kwamba pesa zote za NG-CDF zitatolewa kabla ya kukamilika kwa mwaka huu wa kifedha wa 2022/2023. Pesa hizo zikiingia katika akaunti zetu, tutazisambaza kwa akaunti za maeneo bunge yote 290 bila kuchelewa,” afisa huyo akaeleza.
Source link