
Wakopaji hela kidijitali bado wahangaishwa
NA DANIEL OGETTA
LICHA ya Serikali ya Rais William Ruto kutangaza kuwa itawaondoa Wakenya kutoka kwa minyororo ya kampuni za kutoa mikopo kidijtali, kampuni hizi bado zinawahangaisha raia kwa kutuma maelezo yao kwa kampuni za kuwaadhibu wanaofeli kulipa madeni (CRB).
Mwaka 2022 Dkt Ruto alianzisha Hazina ya Hasla ili kutoa mikopo midogo kwa gharama ya chini kwa Wakenya ambao zamani waliumizwa kampuni zinazomilika apu za kutoa mikopo kupitia simu ya mkononi kwa riba ya juu.
Lakini kufikia sasa bado raia wengi wasiojiweza kifedha huchukua mikopo kupitia apu hizi zinazoendelea kuvuruga maisha yao.
Wakopeshaji hawa pia husambaza jumbe za kupotosha kuhusu Wakenya wanaochelewa kulipa madeni yao.
Wengine hutumia nambari za simu za jamaa na marafiki wa wateja wao ili wakiwataka kuchanga pesa za kuwasaidia kulipa madeni yao.
Mmoja wa wanaohangaishwa na apu hizi ni Bi Stacy Achieng’ (sio jina lake halisi) ambaye alichukua mkopo wa Sh18,290 kutoka kwa apu ya RahisiPesa ili kugharimia matibabu ya dharura ya mamake.
Alipofeli kulipa pesa hizo kwa wakati, wasimamizi wa apu hiyo waliwafikia watu wote walioko kwenye akaunti ya Achieng’ ya mtandao wa WhatsApp na kuwauliza wamchangie pesa za kulipia mkopo wake.
“Hizi ndizo nambari za simu za watu wote ambao wewe huwasiliana nao. Sasa ni heri kundi la WhatsApp liundwe ili marafiki zake wakusaidie.” Wasimamizi hao wakamwandikia Achieng’.
Jamaa na marafiki wa watu wengine waliofeli kulipa mikopo yao pia hutumiwa jumbe za kutisha kama huu: “Aisee, mtu tuliyemtaja hapa alitupa maelezo yako kama mdhamini wake alipochukua mkopo kutoka kwetu. Ikiwa wakati fulani utanyimwa msaada wa kifedha kutoka benki, shirika la mikopo au shirika lolote la kifedha unajua aliyehusika. Utahitajika kuthibitisha kutoka kwa mtu huyo kabla ya sisi kuwasilisha jina lako kwa CRB”.
Lakini kulingana na CreditInfo, mojawapo ya kampuni za CRB zinazohudumu nchini, jumbe kama hizo hazifai kutumiwa marafiki wa watu waliochelewa kulipa madeni yao.
Meneja wa kampuni hiyo anayesimamia ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini katika kampuni ya CrediInfo Steven Kunyiha anasema hivi: “Mbinu kama hii ya kukusanya madeni hairuhusiwi. Ni jambo la kusikitisha kwamba mkopeshaji anatumia habari za uwongo kumshurutisha aliyekopeshwa alipe deni lake.”
Bw Kinyiha anasema kuwasilishwa kwa maelezo ya aliyefeli kulipa mkopo ni mchakato unaosimamiwa na Benki Kuu ya Kenya (CBK). Na ni mkopeshaji aliyepata leseni kutoka kwa asasi hiyo ya kusimamia mashirika ya fedha nchini ndiye anaruhusiwa kuanzisha mchakato huo.
“Kabla ya maelezo ya mtu kutumwa kwa CRB, sharti idhini itolewe. Anayefanya hivyo sharti apate leseni kutoka CBK,” anaeleza.
Moto mkali wazidi kuharibu misitu ya Aberdares na Mau
Source link