
Wito mradi wa gesi wa Taifa uwafaidi wakazi wa Pwani
NA JURGEN NAMBEKA
RAIS William Ruto pamoja na viongozi wengine wakuu serikalini hapo jana Ijumaa walizindua ujenzi wa kiwanda cha kuhifadhi na kusambaza gesi katika eneo maalumu la kiuchumi la Dongo Kundu kaunti ya Mombasa.
Akizungumza katika uzinduzi huo wa mradi utakaomgharimu mwekezaji wa taifa jirani la Tanzania Bw Rostam Aziz Sh 16 bilioni, alimtaka kuhakikisha kuwa mradi huo unawafaidi pakubwa Wapwani.
“Nimefurahi kwa heshima uliyonipa Bw Aziz kuja hapa kuweka msingi wa mradi huu. Ninataka nikuombe kuwa wakazi wa Mombasa, Likoni na Pwani kwa ujumla ndio wanaopata kufaidika kwanza na nafasi za ajira zitakazotokana na uwekezaji huu,” alisema Rais Ruto.
Kulingana na rais, hatua hiyo ya kuwekeza katika eneo la Dongo Kundu kungebadilisha maisha ya Wakenya kwa njia nyingi ikiwemo kupunguza idadi ya watu wanaopika kwa kutumia kuni.
“Idadi ya Wakenya wanaotumia kuni hapa nchini ni asilimia 70 kwa sasa. Mradi huu Bw Aziz tunapongeza kwa kuwa utasaidia kuhakikisha akina mama wanaohangaika jikoni kwa moshi wanapopika wanapata gesi kwa bei nafuu,” akasema.
Suala la kampuni ya Taifa Fuel kutoa nafasi za ajira kwa Wapwani liliungwa mkono na naibu wa Rais Rigathi Gachagua aliyetaka kampuni hiyo kutowaleta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.
“Mimi nataka kuambia wawekezaji wetu kuwa, waanze na hawa watu wa hapa kwa kutoa ajira. Ukija kuzindua kiwanda kuja tu na Meneja na karani wa kuwalipa watu wetu,” alisema Bw Gachagua.
Alimtaka pia mwekezaji huyo, kuwalipa wafanyakazi hao kila wiki badala ya mwezi. Kulingana na Bw Gachagua hii ingewawezesha kupanga hesabu ya matumizi ya majumbani kwao kwa urahisi.
Waziri wa biashara Bw Moses Kuria naye pia alisisitiza kuwa, kulikuwa na umuhimu wa watu wa Pwani kupata ajira, ili kuwawezesha kiuchumi.
Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, aliyehudhuria uzinduzi huo, aliwatetea wakazi wa eneo lake ambako hifadhi hiyo inajengwa, akiwataka wao kupewa kipaumbele kabla ya watu wa maeneo mengine ya Pwani.
Haya yanajiri huku Mkurugenzi Msimamizi wa mradi huo Bi Veneranda Masoum, akieleza kuwa mradi huo utabuni nafasi za kazi 90,000 humu nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bw Aziz alimshukuru Rais Ruto kwa kumaribisha nchini, na kumruhusu kujiunga na sekta ya kuuza gesi ya LPG.
Aidha alieleza kuwa wakati wa ubaguzi wa wanabiashara wa ukanda wa Afrika mashariki kuzuiwa kuwekeza katika nchi jirani ulipaswa kufikia mwisho.
“Nataka nimweleze mheshimiwa Rais Ruto kuwa inahuzunisha sana jinsi ambavyo wanafabiashara wa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wananyimwa nafasi za kuwekeza. Inakuwa rahisi kwa mwekezaji wa kutoka nje ya bara la Afrika kuwekeza kutuliko sisi hapa. Ni wakati wa jambo hilo kukoma,” alisema Bw Aziz.
Bw Aziz alieleza kuwa Wakenya wanaoishi karibu na mradi huo, wangepewa kipaumbele mara tu nafasi za ajira zitakapojitokeza.
Source link